F Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yapata Gawio la Tsh. Bilioni 25 | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yapata Gawio la Tsh. Bilioni 25


Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imepata faida  zaidi ya shilingi bilioni 25 ikiwa ni malipo ya  huduma za matumizi ya mkonga wa taifa, Serikali mtandao Visiwani Zanzibar

Mkurugenzi Mtendaji Wakala wa Mkonga wa Mawasiliano Zanzibar, Mhandisi Shukuru Awadhi Suleiman amesema kwamba fedha hizo zimelipwa kutoka katika makapuni ambayo yanatumia huduma zao.

“Tumepata fedha hizo ambazo kutoka Kampuni ya simu ya ZANTEL ikiwa ni malipo kuanzia mwaka 2013 hadi mwaka 2024” Alisema Mkurugenzi huyo.

Alisema kwamba Serikali mtandao imekuwa na faida kubwa kwa wananchi ambapo sasa huduma za afya, kodi na elimu zimekuwa zikitolewa kwa urahisi na ufanisi mkubwa.

Amesema katika sekta ya afya, kumekuwa na mafanikio makubwa katika huduma, vituo vya afya 24 Unguja na Pemba vimeunganishwa katia mfumo wa Serikali mtandao.

“Leo hii mgonjwa anaweza kufanyiwa vipimo kama vya X-ray katika hospitali ya Kivunge Mkoa Kaskazini Unguja  na, vipimo vile vitasomwa Hospitali kuu ya Mnazi Mmoja bila ya mgonjwa au daktari kulazimika kusafiri” Alisema Mkurugenzi Mhandisi Shukuru.

Mkuruhenzi huyo amesema kwa kutumia huduma za Serikali Mtandao, huduma za vyeti vya kuzaliwa imekuwa rahisi kwa sasa kwani wananchi wanapata vyeti vya kuzaliwa katika Wilaya zao.

“Sasa hivi Wakala wa Usajili na Matukio ya Kijamii Zanzibar wanatumia huduma hizi, watu wanapata vyeti vyao vya kuzaliwa katika Wilaya zao, wanaomba huko na taarifa zao zinatumwa Makao Makuu na kufanyiwa kazi” Alisema Mkurugenzi Shukuru.

Mbali ya sekta hizo, pia Kampuni ya Uunganganishaji Maudhui ya ZMUX inatumia mkonga wa taifa katika kurusha matangazo ya Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).

Akizungumzia sekta ya kodi,  Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema kwamba Bodi ya Mapato Zanzibar ni moja ya watumiaji wakubwa wa huduma za Serikali mtandao ambapo sasa huduma za kodi zimeunganishwa katika mtandao mmoja.

Amesema tayari wamepokea maombi ya makampuni ya simu, TTCL, na kampuni ya Comnet kutaka kutumia huduma za mkonga wa taifa.

Nae Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano, Dkt Mzee Suleiman amesema kumekuwa na mafanikio katika matumizi ya TEHAMA hasa baada ya kukamilika kwa mkonga wa taifa.

Dkt Mzee amesema mwaka 2011, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Ali Mohamed Shein alitoa agizo la kuhakikisha Zanzibar inaongeza kasi ya matumizi ya TEHAMA katika shughuli mbalimbali.

Mkurugenzi huyo amesema kuna vituo 10 vya kuwafundisha wananchi matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano, ambapo mafunzo hayo yanatolewa bure kwa wananchi.