F Shule inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi CCM ipo hatarini kukosa Wanafunzi | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Shule inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi CCM ipo hatarini kukosa Wanafunzi



Na Amiri kilagalila-Njombe

Shule ya sekondari Masimbwe inayomilikiwa na jumuiya ya wazazi CCM wilaya ya Ludewa mkoani Njombe inakabiliwa na changamoto ya kukosa wanafunzi wa kujiunga na shule hiyo pamoja na kupata athari za kitaaluma kutokana na miundombinu mibovu inayosababisha baadhi ya wazazi kuhamisha watoto wao.

 Taarifa ya mkuu wa shule bwana Eliud Godson Sanga kwa wanahabari inasema mpaka sasa  shule ina idadi ya wanafunzi 56 pekee kuanzia kidato cha kwanza mpaka kidato cha nne huku wanafunzi 17 wakihitimu kidato cha nne mwaka huu lakini bado idadi inaonekana kuendelea kupungua kila mwaka.

Muungwana Blog imefika shuleni hapo na kuona changamoto zinazoikabili ikiwemo ukosefu wa miundo mbinu ya umeme,uchakavu wa mabweni hasa kwa watoto wa kike kwani mpaka sasa wanafunzi wa kike wanaosoma katika shule hiyo wanaishi katika bweni lililojengwa kwa mbao,huku baadhi ya wanafunzi waliopo shuleni hapo wakiomba chama cha mapinduzi kuwasaidia kuboresha miundombinu hiyo.


“Changamoto kubwa kwetu sisi wasichana moja ni bweni la wasichana,unakuta wakati mwingine mlango umebomoka kunakuwa hakuna amani ya kuishi katika bweni,lakini pia bweni letu ni la mabanzi hivyo tunakosa amani kwasababu hakuna amani kwa kuwa tunahisi lile bweni muda wowote linaweza likabomolewa,sasa badala ya kuwaza masomo darasani tunawaza nitaishije kule bwenini hali ikiwa ni ngumu kiasi kile.Tunaomba CCM watusaidie kwa hali na mali ili kufanikisha uboreshwaji wa mazingira ya hii shule”alisema mmoja wa wanafunzi wa kike shuleni hapo

Eliud Godson Sanga ni mkuu wa shule ya Masimbwe anakiri kuwa shule yake ina changamoto lukuki huku idadi ya wanafunzi wanaojiunga na shule hiyo ikimshitua.

Aidha anaelezea changamoto zinazo ikabiri shule hiyo ambapo amesema kuwa uwepo wa changamoto hizo unaathiri kwa kiwango cha ukuaji wa elimu katika shule hiyo.

“Wanafunzi hawana umeme,hawawezi kusoma darasani mpaka muda wanaoutaka,anatakiwa asome muda mfupi alale kwasababu umeme unaotumika ni wa sola na wakati mwingine unazima,lakini pia bweni la wasichana hatuna inatulazimu tuwaweke wanafunzi katika bweni la mbao ambalo ni hatari kwa wanafunzi”anasema Eliud Godson Sanga

Hata hivyo mkuu huyo amesema Chama cha Mapinduzi kimeendelea na mikakati ya kuimarisha shule zao zote kwa kuwa tayari tume maalumu kutoka taifa imekwisha pita shuleni hapo zaidi ya mara mbili na kuandika yanayohitajika katika shule hiyo lakini kwa upande wake amekwisha fanya kazi kwa upande wake ikiwemo kuomba vifaa kwa hisani hivyo changamoto kubwa katika shule hiyo ni miundombinu ya majengo na sio swala la vifaa.

Edger Mtitu amekuwa mgeni rasmi katika mahafari ya 23 iliyofanyika Novemba 20 mwaka huu shuleni hapo  anasema hali ya shule hiyo kwa sasa ni mbaya kutokana na kukosa wanafunzi wa kujiunga na shule huku akiahidi kugharamia matangazo ili kufanikisha zoezi la upatikanaji wa wanafunzi

“Shule hii siyo ya kuwa na kidato cha nne wanafunzi wanne tu,haiwezekani kabisa moja ya vitu ambavyo mimi nitavifanya katika shule hii nitajitolea kufanya matangazo,lakini natoka na baadhi ya changamoto kwa ajili ya kuwashawishi wenye mamlaka husika ili hii shule iludi kwenye misingi ya zamani,kwasababu wazazi walikuwa wanatuleta kujifunza kwenye shule hii lakini sahizi wanapelekwa sehemu nyingine, haiwezekani”alisema Mtitu

Shule ya sekondari Masimbwe ilianzishwa mwaka 1994 ikiwa chini ya jumuiya ya wazazi ccm wilaya ya ludewa ambapo mpaka hivi sasa ni miaka 25 tangu kuanzishwa kwake.