Idadi ya watu waliofariki kwenye mkasa wa maporomoko ya udongo nchini Kenya imeongezeka hadi 46 huku shughuli za uokoaji na kutafuta miili ya waathiriwa zikiendelea.
Aidha gazeti la Nation limeripoti hii leo kwamba watu 400 wamebaki bila makazi kufuatia mkasa huo uliotokea Ijumaa usiku katika kaunti ya Pokot magharibi, kaskazini magharibi mwa Kenya.
Gazeti hilo limemnukuu gavana wa eneo hilo John Lonyangapuo akielezea hofu kwamba idadi ya waliofariki huenda ikapanda.
Serikali imetuma helikopta za polisi na jeshi kusaidia katika shughuli ya kutafuta manusura na miili ya waathiriwa.