Rais John Magufuli leo ameweka rasmi mawe ya msingi katika miradi ya ujenzi wa Chelezo, Meli mpya na ukarabati wa Meli ya Mv Victoria na Butiama.
Katika hafla hiyo Rais Magufuli ameipongeza Kampuni ya Huduma za Meli kwa kazi nzuri na kuunga mkono wazo la Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo Eric Hamissi la kununua Meli ya kwenda Comoro.
Meli mpya ambayo ujenzi wake umezinduliwa leo itakuwa ni kubwa kuliko Meli zote Tanzania na Nchi jirani katika ukanda wa Maziwa Makuu. Itafanya safari zake kati ya Mwanza na Bukoba kupitia Bandari ya Kemondo pia Mwanza na Musoma, na safari kati ya Mwanza na Kenya na Uganda.
Meli hiyo itakuwa na urefu wa Mita 92.6, upana ni Mita 17 na kimo chake ni Mita 11.2, na itakuwa na Madaraja 3, Daraja la kwanza litabeba abiria 50, la pili abiria 316 na la tatu litabeba abiria 834.
Meli mpya ya abiria na mizigo katika Ziwa victoria ambayo pia Rais Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wake ikikamilika kwa ujumla itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1200, tani 400 za mizigo, magari makubwa 3 na madogo 20.