Waharibifu wamekata pua ya sanamu ya gwiji wa soka Zlatan Ibrahimovic nje ya uwanja wa Malmo nchini Sweden.
Ni kitendo cha hivi karibuni cha uharibifu kilichoilenga sanamu hiyo tangu itangazwe kwamba Ibrahimovic alikuwa amewekeza katika klabu pinzani mwezi uliopita.
Mshambuliaji wa zamani wa Sweden Ibrahimovic ,38, alianza kushiriki katika soka ya kulipwa akiichezea Malmo miaka 20 iliopita.
Msanii aliejenga sanamu hiyo Peter Linde amewaomba raia kutoiharibu.
Mchezaji huyo wa zamani wa Ajax , Juventus, Intermilan , Barcelona, Milan, PSG na Man United anatafuta klabu atakayojiunga nayo baada ya kuondoka LA Galaxy mwisho wa msimu wa MLS.
Tarehe 27 Novemba , ilitangazwa kwamba alikuwa amenunua asilimia 25 ya hisa za klabu ya Hammarby, ambayo ilimaliza ya tatu katika ligi ya mwaka huu ya Sweden.
Siku hiyo hiyo , sanamu hiyo ya shaba yenye urefu wa mita 3.5 , iliozinduliwa na Shirikisho la soka nchini Sweden ilipuliziwa rangi , kuchomwa huku kiti cha choo kikiwekwa katika mkono wake .
Nyumba ya Ibrahimovic mjini Stockholm pia iliharibiwa huku jina 'Judas' likiandikwa katika mlango wake wa mbele.