F Kanisa katoliki lasema kutekeleza miradi ya kutolea huduma za kijamii ni sehemu ya wajibu wake | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Kanisa katoliki lasema kutekeleza miradi ya kutolea huduma za kijamii ni sehemu ya wajibu wake

Na Ahmad Mmow, Nachingwea.


Pamoja na kufundisha, kuhubiri na kutangaza habari njema kwa binadamu na viumbe vyote duniani, lakini pia kanisa linaendelea kutimiza wajibu wake wa kutekeleza miradi ya kutolea huduma za kijamii. Ikiwa ni sehemu ya upendo ambao unahubiriwa na kanisa hilo.

Hayo yameelezwa leo na mhashamu Askofu, Bruno Ngonyani wa jimbo katoliki la Lindi, wakati wa hafla ya kubariki majengo ya shule ya awali na msingi. Shule ambayo inamilikiwa na masista wa ki-Afrika wa Benektini wa Ndanda.

Mhashamu Askofu Ngonyani ambae aliongoza ibada ya kubariki shule hiyo alisema kanisa kujenga majengo ya  kutolea huduma za jamii na miradi mingine ya kijamii ni sehemu ya wajibu wake wa msingi. Licha ya kuhubiri na kutangaza utukufu wa Mungu kwa viumbe vyote.

Alisema hata wamisionari walipokuja kuhubiri habari njema hapa nchini hawakuishia kufanya kazi hiyo tu. Bali walifanya kazi nyingine ikiwa ni sehemu ya wajibu wa kanisa. Ikiwamo kujenga majengo na kutekeleza miradi ya kutolea huduma za kijamii.

" Kwakuwa kanisa ndio kristo, naye kristo pamoja na kuhubiri , kutangaza habari njema na wokovu lakini alifanya uponyaji na kufundisha. Nasisi tunafuata nyayo zake. Kwani ndio wajibu wa kanisa ambalo limekuwa likitangaza na kuhubiri upendo. Na upendo ni kusaidia watu wenye uhitaji," alisema mhashamu Askofu Ngonyani.

Alibainisha kwamba kwakufanya hivyo sio tu kwamba kanisa litakuwa linatimiza wajibu wake wa msingi, bali pia litatakuwa linaisadia serikali kutekeleza nia njema ya kutoa huduma bora za jamii kwa wananchi wake, tena bila ubaguzi.

Mbali na hayo, mhashamu Askofu Ngonyani alitoa wito kwa waamini wa dhehebu hilo, wakristo na wananchi kwa jumla wafanye kazi kwa bidii na maarifa kwa faida yao na taifa. Akiweka wazi kwamba kazi ni sehemu ya wajibu wa maisha ya binadamu.

" Kazi zinafanywa kwa kutumia vipawa. Na akili ni kipawa, akili hizo ndizo tunatumia kutambua na kuchagua kati ya mema na mabaya. Kufanya kazi ni sehemu ya uchaguzi wa mema, natunatakiawa kuziendeleza ili tuweze kufanya kazi kwa ufanisi kwa faida yetu na kwa wengine, ndio kutekeleza upendo kwa vitendo," alisisitiza Ngonyani.

Ujenzi wa shule hiyo ambayo hadi kukamilika umefanywa na wamiliki wa shule hiyo, ambao ni masista wa ki- Afrika wa Benediktini wa Ndanda.