Na John Walter, Babati
Shirika lisilo la Kiserikali,Siasa,dini wala biashara la Community Support Initiatives Tanzania (Cosita) katika mipango mikakati yao inayoishia mwaka 2021 limelenga kuhamasisha Jamii kujenga mabweni ya wasichana katika shule za kata katika Halmashauri ya mji wa Babati mkoani Manyara.
Mkurugenzi wa shirika hilo Patrice Gwasma amesema wameamua kufanya uhamasishaji huo wa ujenzi wa Mabweni kwa watoto wa kike katika shule za sekondari baada ya kugundua kuwa wengi hukatisha ndoto zao kwa kurubuniwa wakati wa kwenda shule au kurudi kwa lifti au pesa kutokana na umbali mrefu wanaotembea kufuata shule.
Amesema katika mpango huo wataanza na shule ya Sekondari Sigino ambayo wanafunzi wake hutoka umbali mrefu wa wa kuanzia kilomita 6 hadi zaidi ya 10.
Mkuu wa shule ya Sekondari Sigino Mwalimu Augusino Burra ametaja umbali wanaotoka wanafunzi wa shule hiyo ambao wanatoka katika vijiji vya Sigino (Km 6), Daghailoi (Km 7), Singu (Km 10), Imbilili (Km12) na kijiji cha Wangbay (Km 13).
Aidha amesema wanafunzi walioacha shule kwa kupata uja uzito kwa Kipindi cha mwaka 2016 wanafunzi wawili,2017 mwanafunzi mmoja, 2018 mwanafunzi mmoja na Mwaka 2019 ni Mwanafunzi mmoja ambaye aligundulika na mimba miezi miwili kabla ya mtihani wa mwisho wa kuhitimu kidato cha nne ambao jumla yao wanafikia wanafunzi Watano.
Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Mji wa Babati Pascalina Lowokelo amsesema ni mwanzo mzuri waliokuja nao Shirika la Cosita kwa ajili ya ukombozi wa Mtoto wa kike hivyo jamii na wote wenye mapenzi mema na wanafunzi wa kike waunge mkono kampeni hiyo.
“Watoto wote wanatakiwa kulindwa lakini linapokuja suala la mtoto wa kike linahitaji ulinzi zaidi kwa sababu wao hupitia mambo mengi tofauti na wa kiume” alisisitiza afisa huyo.
Amesema juhudi za shirika la Cosita zitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la Mimba za utotoni na kuongeza Ufaulu kwao.
Aidha takwimu za Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya Tanzania wa Mwaka 2015-16 zinaonyesha kuwa, asilimia 27 ya wanawake vijana wenye umri wa miaka 15-19 tayari wana watoto au ni wajawazito tayari.