F Mkurugenzi Jiji la Dodoma akabidhi magari kwa wataalam wake kukabiliana na ujenzi holela | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Mkurugenzi Jiji la Dodoma akabidhi magari kwa wataalam wake kukabiliana na ujenzi holela

Halmashauri ya Jiji la Dodoma limekabidhi magari matatu kwa Idara ya Mipango Miji kwa ajili ya kurahisisha shughuli za wataalamu wake katika kudhibiti ujenzi holela kwenye jiji hilo.

Hayo yamefanyika ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Mhe Kassim Majaliwa la kusimamia utekelezaji wa mpango kabambe wa Jiji la Dodoma.


Akizungumza wakati wa kukabidhi magari hayo, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi amesema magari hayo yamegharimu kiasi cha Sh Milioni 345 kwa idara ya mipango miji ambapo yatatumiwa na ofisi ya udhibiti ujenzi holela, mkuu wa upimaji na mkuu wa idara ya mipango miji.

Kunambi amesema halmashauri ya jiji inaamini ili kutekeleza agizo la Mhe Waziri Mkuu ni lazima wawe na vitendea kazi ambavyo vitarahisisha ufanyaji kazi wa watalaamu wao.

" Mhe Mkuu wa Mkoa tunakushukuru kwa kuja kwenye tukio letu hili, haya ni mafanikio makubwa kwetu katika kuondoa changamoto ya vitendea kazi kwa wataalamu wetu ambao wanakua field muda wote kuhakikisha wanaondoa tatizo la ujenzi holela kwenye jiji letu.

Fedha hizi Milioni 345 ni fedha zetu za mapato ya ndani, Jiji la Dodoma hatuombi fedha serikali kuu kama halmashauri zingine. Sasa tunaamini hakuna nyumba yoyote ambayo itawekea X kwa sababu kabla hata ya kujenga wataalamu wetu watakua wameshatoa elimu kwa wananchi juu ya maeneo gani ya kujenga na ya yapi hayafai kujenga," Amesema Kunambi.

Ameongeza kuwa Jiji la Dodoma linapiga hatua kutokana na ushirikiano uliopo baina ya Ofisi yake, Mkuu wa Wilaya pamoja na Baraza la Madiwani linaloongozwa na Mstahiki Meya, Prof Davis Mwamfupe.

" Mhe RC hakuna Jiji lingine ambalo limepangwa vizuri kwa asilimia 100 zaidi ya Jiji letu la Dodoma, lakini pia Jiji letu limepimwa kwa asilimia 60 hatutaki kabisa kuharibu madhari ya Jiji letu na tunakuhakikishia mpango kabambe tuliokabidhiwa na Mhe Waziri Mkuu tutautekeleza kwa asilimia 100," Amesema Kunambi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge amelipongeza jiji hilo kwa kupiga hatua ya kuwanunulia watalaamu wake magari ambayo pia yatakua msaada kwa wananchi waliokua wanasafiri umbali mrefu kufika ofisi za Jiji.

" Sitegemei kuwaona watalaamu ofisini, hizi gari tunazowakabidhi leo zitumieni vizuri kwa kwenda field walipo wananchi, muwape elimu nzuri ili kuepusha changamoto za baadae za ujenzi holela.

Hatutaki tena kuona ujenzi holela, wala kuona alama za X maana zikiendelea kuwepo zinatoa picha kwamba nyie watalaamu wetu hamfanyi kazi ipasavyo licha ya kukabidhiwa magari mazuri yanayorahisisha utendaji kazi wenu," Amesema Dk Mahenge.

RC Mahenge amelitaka Jiji la Dodoma kuhakikisha linaondoa pia changamoto ya wananchi kujenga kwenye maeneo ya wazi, milima pamoja na maeneo ya hifadhi.