F Mkuu wa Magereza Tanzania aanza kutekeleza agizo la Rais la kujitegemea. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Mkuu wa Magereza Tanzania aanza kutekeleza agizo la Rais la kujitegemea.

Na John Walter-Manyara.
MKUU wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishna Jenerali Suleiman Mzee, amesema kuwa Jeshi hilo limeanza mikakati ya kuanza kujitegemea kupitia rasilimali zake ikiwa ni agizo la Rais Dkt. John Magufuli.

Amesema  Jeshi hilo lina uwezo mkubwa wa kutumia rasilimali zake zilizopo ndani ya Jeshi la Magereza, ambazo zinaweza kuliwezesha kujitegemea bila kutegemea bajeti ya Serikali.

Kamishna Jenerali Suleiman Mzee amesema hayo leo Jumapili March 1,2020 akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Manyara ambapo amemtaka mkuu wa Magereza mkoani hapo kuhakikisha wanaanzisha miradi mbalimbali itakayowawezesha kuingiza kipato badala ya  kutegemea mafungu ya serikali.

Ameongeza kuwa Magereza kujitegemea inawezekana kwa sababu wanazo rasilimali nyingi ikiwemo mashamba ya kilimo, mifugo,rasilimali watu ambao ni wafungwa na wataalam ambapo zikisimamiwa vyema na kuachana na ubinafsi wataliwezesha Jeshi hilo kujitegemea.

Aidha, Kamishna Jenerali Suleiman Mzee alitembelea mashamba ya Magereza na ujenzi wa nyumba za watumishi zilizoanza  kujengwa kwa nguvu za jeshi Magereza mkoani Manyara. Kamishna Jenerali wa Magereza Tanzania anaendelea na  ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo  inayosimamiwa na Magereza.