F Kanisa la Mlima wa Moto watangaza wiki ya maombelezo | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Kanisa la Mlima wa Moto watangaza wiki ya maombelezo

MCHUNGAJI Kiongozi wa Kanisa la Mlima wa Moto lililopo Sabasaba Jijini Dodoma, Slivanus Komba ametangaza maombi ya Maombolezo ya siku saba ikiwa ni sehemu ya kumuenzi Dk. Getrud Rwakatale.

Mchungaji Komba ambaye pia ni Askofu wa Kanda ya Kati na  Nyanda za Juu kusini amesema lengo la maombolezo hayo ni kumuenzi kwa vitendo kutokana na mema na maonyo alikuwa akiyatenda mbeba maono wa Kanisa hilo na aliyekuwa askofu mkuu wa Kanisa la Mlima wa Moto Tanzania, Marehemu Mch. Rwakatale.

Askofu Komba alisema pamoja na kutangaza maombolezo ya siku saba ya Kanisa hilo pia litaendelea na maombolezo ya siku 40 ambayo yametangazwa kitaifa na Kanisa hilo ambayo yatakuwa ya kitaifa.

Kiongozi huyo wa Kiroho alisema kuwa kibiblia hakuna kioongozi yeyoye wa kidini ambaye anaweza kufanya maombolezo kwa ajili ya kumshawishi Mungu kubadilisha mawazo ya mtu aliyekufa kumpeleka peponi au motini kulingana na kile ambacho alikitenda akiwa hai.

Alisema wakati wa uhai wa Mch. Dk. Rwakatale alikuwa ni mstari wa mbele katika kuhakikisha kazi ya Mungu inasonga mbele licha ya kuwa alikuwa mfanyabiashara mkubwa na mwanasiasa.

Katika ibada hiyo ambayo ilikuwa ya tofauti ambayo ilighubikwa na majonzi vilio kwa washirika wa kanisa hilo, Askofu Komba aliwataka waumini wote kuhakikisha wanahudhuria Ibada zote za siku bila kukosa ikiwa ni sehemu ya maombolezo.

Katika hatua nyingine, Askofu Komba amekemea baadhi ya uzushi juu ya wanaopakaza kuhusu mrithi wa Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo.

“Pamoja na kuwa Mimi siyo msemaji wa Kanisa hili wapo wasemaji lakini nipende kusema kuwa kwa sasa tupo katika kipindi kigumu cha kuondokewa na Kiongozi wetu mbeba maono.

“Nashangaa kwa mtu yeyote ambaye anawaza kurithi sisi hatupo kwa ajili ya kurithi, tunawaza kufanya kazi ya Mungu na kwa sasa Kanisa lipo ya Baraza la wazee.

“Kwa mtu ambaye anawaza kurithi hana nia njema na huduma ya kuifanya kazi ya Mungu bali maamuzi yote yatatolewa na Baraza la wazee wa kanisa baada ya siku 40,” alisema Askofu Komba.