Na Ahmad Mmow, Lindi.
Chama kikuu kikuu cha ushirika cha Lindi Mwambao kinatarajia kugawa vipimo vya kupima unyevu na mizani ndogo kwa wanachama wake( AMCOS) kabla ya mwezi Oktoba, mwaka huu.
Hilo limeelezwa na meneja mkuu wa chama hicho, Nurdiin Swallah alipozungumza na Muungwana Blog, leo mjini Lindi baada ya kuombwa atoe maoni yake kuhusu mipango ya chama hicho kuunga mkono kwa vitendo mpango wa serikali wa kufanya nchi iwe ya viwanda na uchumi wa kati.
Alisema chama kikuu hicho kinatambua na kuunga mkono mikakati na mipango ya serikali ya kuwainua wananchi na taifa kiuchumi. Ikiwa nipamoja na mpango wa nchi ya viwanda na uchumi wa kati. Kwahiyo kitaanza na kugawa mizani ndogo na vipimo vya kupima unyevu kwenye korosho ili zitakazo nunuliwa kutoka katika chama hicho ziweze kumudu ushindani wa soko.
Alisema mpango huo ambao ni utekelezaji wa agizo la serikali kwa vyama vikuu vya ushirika kupitia vikao viwili vilivyofanyika hivi karibuni baina yao na naibu waziri wa wizara ya kilimo, mheheshimiwa Hussein Bashe( Mb) unatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Oktoba mwaka huu.
Alisema chama hicho kinatambua azima ya serikali ya kuyaongezea thamani mazao ya kilimo kutoka kuwa mazao ghafi na kuwa bidhaa. Hata hivyo kimeamua kuanza kutekeleza mpango huo kwa nguvu zote. Kwani kinatambua kwamba ubora wa bidhaa unaanzia kwenye ubora wa mazao.
Alisema serikali inamipango mizuri ya kuwainua wananchi kiuchumi kupitia raslimali zilizopo katika maeneo wanayoishi, ambayo ni fursa wanazoweza kutumia kuinua vipato vyao na kushiriki kikamilifu ujenzi wa uchumi wa nchi. Hata hivyo azima hiyo ya serikali itafanikiwa iwapo kutakuwa na usimamizi na ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wake.
" Kwamfano shirika la viwanda la kuhudumia viwanda vidogo( SIDO) linajitahidi sana kutekeleza wajibu wake. Limeanzisha mkakati unaotambulika kwa jina la "WILAYA MOJA BIDHAA MOJA". Mkakati huo ukisimamiwa vizuri, na wananchi wakifanyia kazi utakuwa na matokeo makubwa," alisema Swallah.
Alitoa wito kwa SIDO ifuatilie kwakaribu utekelezaji wa mpango huo na mingine na ikutane mara kwa mara na taasisi washirika na shirika hilo. Ikiwamo shirika la viwango la taifa( TBS) ili kujadili na kupata njia za kupunguza nahata kuondoa yote ambayo yanaonekana ni kikwazo kwa wajasiriamali kushiriki mpango wa serikali wa kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati.
Aidha meneja mkuu huyo wa Lindi Mwambao alitoa wito kwa wananchi watumie fursa zinazo wazunguka. Akiweka wazi kwamba wilaya ya Lindi imefanya jambo jema chagua unga wa muhogo kuwa bidhaa ya kimkakati. Akiweka wazi kwamba uamuzi huo umepanua wigo na fursa nyingine kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Alisema mihogo, mbaazi, alizeti na kunde yanaweza kuwa mazao ya biashara mbadala wa korosho na ufuta iwapo masoko ya korosho na ufuta yataporomoka kutokana na sababu mbalimbali. Huku akitoa wito kwa wakulima kuanza kujaribu kulima kahawa katika maeneo yanayoonesha dalili za kustawi vizuri zao hilo.