Waziri Hasunga kwa kushirikiana na TAHA aongoza wadau wa Horticulturemapokezi ya ndege ya mizigo uwanja wa KIA

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) kwa kushirikiana na Asasi kilele ya kukuza na kuendeleza kilimo cha matunda, mboga, maua na mbegu Tanzania (TAHA) Kadhalika kampuni ya kuendeleza kiwanja cha ndege cha Kilimanjaro (KADCO) ameongoza mapokezi ya ujio wa ndege ya mizigo kwa ajili ya kutatua changamoto ya usafirishaji wa mazao kwenda nje ya nchi.


Ndege hiyo aina ya 787-Dreamliner ambayo ni mali ya shirika la ndege la Ethiopia imekuja kwa kuitikia jitihada za serikali inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli kupitia wizara ya Kilimo pamoja na TAHA ambayo ilikuwa na jitihada ya muda mrefu ya kutafuta namna ya kutatua changamoto ya kuokoa hasara inayokuwa inatokea kwa wakulima kutokana na madhara ya ugonjwa wa homa ya mapafu wa COVID-19.


Akizungumza wakati wa mapokezi hayo yaliyofanyika katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) Leo tarehe 17 Aprili 2020 majira ya jioni Waziri Hasunga amesema kuwa madhara ya ugonjwa huo yamesababisha makampuni mengi ya ndege duniani kusimamisha safari za ndege hivyo kusababisha madhara makubwa kwa wakulima na wafanya biashara wa mazao mbalimbali ikiwemo Matunda, Mboga, Maua na Mbegu.

Waziri Hasunga amesema kuwa Ndege hiyo ya mizigo itakuwa ikitua mara tatu kwa wiki kwa ajili ya kupakia mizigo ili kusafirisha, jambo litakalopunguza adha kubwa kwa wakulima waliokuwa wakiteseka na kutafuta nafasi za kusafirisha mazao yao katika nchi jirani.

Hasunga amesema kuwa hiyo ni mara ya kwanza kwa mazao hayo kutoka Tanzania kuingia moja kwa moja kwenye soko la Ulaya na serikali imefanikisha kuondoa kabisa tatizo la masoko Kadhalika serikali inaendelea na mazungumzo na Shirika la ndege la Emirates ili kuanza kupeleka mizigo katika soko la Asia na kwingineko ikiwemo nchi za Uarabuni.


Pia amebainisha kuwa Serikali imechukua hatua mahususi za kuyarudisha Makampuni yote yaliyokuwa yanazalisha mboga, Maua na Matunda lakini yakasimama kutokana na changamoto mbalimbali ili yaendelee na uzalishaji na ndege zitakazoendelea kuja ziweze kupata mizigo mbalimbali.

Katika hatua nyingine Waziri Hasunga ameahidi kuwa serikali itazipitia Tozo mbalimbali ili kuwe na mvuto wa kibiashara na wakulima nchini kuendelea kuneemeka na fursa hiyo ya uwekezaji katika kilimo hicho cha kibiashara.


Akizungumza mara baada ya kutua kwa ndege hiyo katika uwanja wa ndege cha kimataifa cha Kilimanjaro, Afisa Mtendaji Mkuu wa TAHA, Dkt Jacqueline Mkindi ameishukuru serikali kwa kuunga mkono jitihada hizo na wadau wengine katika kutafuta suluhisho la changamoto zainazowakabili wakulima wa sekta ya Mboga, Maua na Matunda.

Amesema kuwa kwa mara ya kwanza Ndege hiyo ilitua nchini Tarehe 9 Aprili 2020 huku ikiondoka na jumla ya Tani 27 za mizigo ya Mazao hayo ya mbogamboga na Matunda na huku ikiwa na KIlogramu 308 za mizigo ya kawaida.

Dkt Mkindi amesema kuwa ili ndege hiyo iendelee kuja na zingine zivutiwe kuja Tanzania serikali inapaswa kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo kuweka mazingira wezeshi kuhakikisha kuwa ndege hizo zinakuja kwa gharama nafuu wanapotua kwa ajili ya kubeba mizigo.

Sambamba na hayo Dkt Mkindi ameishauri serikali kuruhusu kibali cha muda mrefu cha kutua kwa ndege hiyo ili kuondokana na uombaji wa kibali kila ndege inapotua kwani gharama ni kubwa.

Hafla ya mapokezi ya ndege aina ya 787-Dreamliner mali ya shirika la ndege la Ethiopia imehudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Kilimajaro Mhe Anna Mghwira pamoja na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi Mhe Atashasta Nditiye.