Na Hamisi Abdulrahmani,Masasi
TAASISI mbalimbali za serikali na kijamii wilayani Masasi mkoani Mtwara zimepokea shehena ya vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa corona ikiwemo Tanki ndogo za maji, barakoa,ndoo za kunawia maji pamoja na vitakasa mikono.
Shehena ya vifaa hivyo vya kujikinga na ugonjwa wa corona vimetolewa jana wilayani Masasi kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mtwara,Gelasius Byakanwa ikiwa ni vifaaa ambavyo vimekuwa vikitolewa na wadau mbalimbali wa maendeleo mkoani Mtwara ambao wanaunga mkono jitihada za serikali katika kujikinga na ugonjwa wa covid-19
Akisoma taarifa ya mapokezi ya vifaa hivyo kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Mtwara, mkuu wa wilaya ya Masasi,Selamani Mzee alisema kutolewa kwa vifaa hivyo kwa taasisi za serikali na kijamii kunalenga kusaidia juhudi za kujikinga na ugonjwa wa corona ndani ya mkoa wa Mtwara.
Alisema vifaa hivyo ambavyo vimetolewa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mtwara ni ndoo za maji 30,stendi za kuwekea ndoo maji 30,barakao 300 boksi mbili za sabuni za kutakasa mikono pamoja na tanki ndogo za kuwekea maji saba.
Mzee alisema taasisi za serikali ambazo zimepokea vifaa hivyo vya kujikinga na ugonjwa huo ni Jeshi la Polisi, Magereza, uhamiaji, Zimamoto, JWTZ,halmashauri pamoja na ofisi ya mkuu wa wilaya.
Aidha,Mzee alisema maeneo mengine ya kijamii ambayo pia wamepokea vifaa hivyo ni Soko kuu la wafanyabiashara la Mkuti Masasi, Soko la Tandale, Soko la Soko sela, Stendi kuu ya mabasi ya Masasi pamoja na maeneo mengine ya yenye mkusanyiko wa watu.
Alisema vifaa hivyo pia vitapelekwa kwenye vijiwe vya bodaboda na sehemu zote ambazo zimekuwa na mkusanyiko wa makundi ya watu lengo kuu ni kuhakikisha kila mmoja anaweza kuchukua hatua na kujikinga na ugonjwa wa corona.
Mzee alisema kutolewa kwa vifaa hivyo kwenye taasisi za serikali na maeneo yale ya kijamii havitolewi kama maonyesho bali vinatolewa kwa ajili ya matumizi mahususi ya kujikinga na maabukizi ya covid-19
“Tunawaomba wadau wengine mbalimbali kuweza kujitokeza kuchangia vifaa kama hivi ili sote kwa pamoja tuwe kitu kimoja katika mapambano haya ya kujikinga na corona tunawashukuru hawa waliochangia vifaa hivi kupitia ofisi ya mkuu wa mkoa Mtwara,”alisema Mzee
Alisema anatoa wito kwa jamii wilayani Masasi kuendelea kuchukua hatua dhidi ya ugonjwa huu wa corona ikiwa ni sambamba na kufuata maelekezo ya wizara ya afya ikiwemo kuepuka mikusanyikoa pamoja na kuvaa barakoa na kukaa umbali wa mita zaidi ya mita moja.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya taasisi za serikali afisa utumishi wa halmashauri ya mji Masasi Gresha Sanga ambaye alimuakilisha mkurugenzi wa halmashauri hiyo ya mji Masasi alisema wanaishukuru ofisi ya mkuu wa mkoa kwa kutoa vifaa hivyo vya kujikinga na corona.
Alisema vifaa hivyo wanakwenda kuvitumia kama ilivyokusudiwa kwenye maeneo yao kwa vile maeneo hayo ni sehemu ambazo wamekuwa wakikutana na watu wengi ambao wamekuwa wakifika kupata huduma za jamii.