F Dawa ya kutibu malaria ya hydroxychloroquine sio tiba ya Corona | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Dawa ya kutibu malaria ya hydroxychloroquine sio tiba ya Corona

Dawa ya kutibu malaria ambayo imefanyiwa majaribio ya uwezo wake wa kutibu virusi vya corona hainusuru maisha ya watu, majaribio makubwa kuwahi kufanyika duniani yabainisha.

Dawa ya Hydroxychloroquine imekuwa ni yenye kupata angalizo kubwa kuhusu uwezo wake wa kutibu virusi vya corona baada ya Donald Trump kuipigia debe kisha kukatokea utata baada matokeo ya utafiti wa dawa hiyo yaliyokuwa yamechapishwa mitandaoni kuondolewa.

Majaribio ya dawa hiyo ambayo yalikuwa yanaongozwa na Chuo Kikuu cha Oxford kwa wagonjwa wenye virusi vya corona kwa sasa hivi yamesitishwa nchini Uingereza.

Utafiti juu ya dawa hiyo umekabidhiwa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Mwanzoni kwa janga la corona, utafiti wa maabara ulionesha kwamba dawa ya kutibu malaria huenda ikaathiri virusi. Utafiti mdogo uliofanywa na China na Ufaransa ukaonesha kwamba inaweza kusaidia wagonjwa.

Kulikuwa na matumaini makubwa kwasababu dawa hiyo ni rahisi na pia imekuwa salama katika matumizi ya kutibu ugonjwa wa malaria na magonjwa mengine kama mapaku mekundu ngozini (lupus) na ule wa yabisi kavu (arthritis).

Hata hivyo, ushahidi wa kuunga mkono matumizi ya dawa hiyo kutibu virusi vya corona yamekuwa hafifu siku baada ya siku.

'Sio dawa ya ugonjwa wa Covid-19'
Hiyo ndio sababu data inayoonesha waliopona ni muhimu. Ni ya kwanza kufanyiwa majaribio kwa idadi kubwa ya watu waliokuwa hospitali.

Zaidi ya wagonjwa 11,000 wa Covid-19 wanashiriki kwenye majaribio huku wagonjwa 1,542 wakipewa dawa ya hydroxychloroquine.

Kwasababu ya utata unaotokana na matumizi ya dawa hiyo ambao unazidi kuongezeka, wadhibiti wa dawa hiyo Uingereza, jana usiku waliomba watafiti kutoka Oxford kupitia tena data yao.

Matokeo yalionesha kwamba asilimia 25.7 ya watu wanaotibiwa kwa dawa ya hydroxychloroquine walikufa ndani ya siku 28. Ikilinganishwa na asilimia 23.5 ya wagonjwa waliopewa matibabu ya kawaida hospitalini.

"Hii sio dawa ya Covid-19," amesema Profesa Martin Landray, ambaye anashiriki majaribio ya dawa hiyo. Mara moja matumizi ya dawa hiyo yakasitishwa.