F Klabu ya wapinga Rushwa VETA Manyara yaja na mipango mipya | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Klabu ya wapinga Rushwa VETA Manyara yaja na mipango mipya



Na John Walter-Manyara

Klabu ya wapinga Rushwa katika chuo cha ufundi stadi (VETA) Mkoa wa Manyara imesema katika kipindi cha mwaka 2020, imejipanga kuhakikisha vitendo vya rushwa vinatokomezwa kwa vitendo.

Hayo yameelezwa na mwenyekiti wa Klabu ya wapinga Rushwa katika chuo cha ufundi Stadi Manyara  (VETA) Juma Manyanya wakati wa hafla fupi ya kuwakaribisha wanachama wapya katika klabu hiyo iliyofanyika chuoni hapo.


Amesema  katika kufanikisha hilo wameandaa mpango wa  kutoa elimu ya umuhimu wa kupinga rushwa kwa wanafunzi wenzao, kila siku asubuhi wakiwa wamekusanyika  kabla ya kuingia  darasani hutoa elimu hiyo kwa ufupi.

Manyanya ameeleza kuwa  wanao mpango wa kufanya ziara za midahalo juu ya kupinga rushwa katika shule na vyuo jirani wilayani Babati.

Pamoja na hayo amesema Klabu ya wapinga rushwa VETA Manyara, imeandaa bustani ya  miti mbalimbali ya kuuza,kuwa na mfuko wa tawi la Klabu rushwa Veta Manyara pamoja na kuwa na sare  (Fulana)  kwa kila mwanachama.

Mwenyekiti  huyo amempongeza Rais John Magufuli na serikali yake kwa namna alivyopambana na rushwa huku akiahidi kuwa wataendelea kuhamasishana katika vita hivyo.


Kwa upande wa mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma kutoka Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU)  mkoa wa Manyara  Sultan Ng’aladizi amesema Pamoja na mafanikio ya TAKUKURU huo  yanayotokana na elimu waliyoitoa kwa jamii juu ya mapambano hayo,Taasisi hiyo pia imeendelea kuvitembelea vilabu vya kupinga Rushwa  katika shule na Vyuo ili kuwajengea uwezo.

 Amesema rushwa inaweza kuzuia nchi isifike kwenye uchumi wa kati wa viwanda kama nguvu ya pamoja na ushirikiano hautakuwepo kuikabili,  hivyo kwa kushirikisha wanafunzi wa vyuo mbalimbali hapa nchini itasaidia kwa kiwango kikubwa suala la rushwa kupotea katika jamii.

Alisema vita dhidi ya rushwa ni tatizo la jamii na dunia hivyo Serikali pekee pamoja na mafanikio iliyoyapata, haiwezi kuimaliza bila kushirikisha wanafunzi katika ngazi zote za msingi hadi vyuoni.

Amewatia moyo wanafunzi hao kwa kuwaeleza kuwa katika vita dhidi ya rushwa kuna vikwazo vingi  lakini ni Lazima wapambane kuanzia sasa ili kuikabili.

Amewaeleza kuwa “kila jambo linawezekana, hivyo  rushwa kumalizika inawezekana  lakini mapambano bado yanahitajika  kwa nguvu kubwa  ya pamoja ili kuhakikisha inatokomezwa”.

Amesema Maadili sio karama kwamba mtu anatunukiwa bali ni mtu mwenyewe kuamua.

 Alisema Rushwa ni adui aliyejiwekea mizizi anayeendelea kuathiri maisha ya mwanadamu na hufanyika kwa siri ndio maana ni ngumu kumkabili, rushwa inasababisha wananchi kukosa imani na serikali yao, inaongeza matabaka ambapo walio masikini huumia zaidi hivyo wanafunzi wakiwa na uelewa itarahisisha kumuondoa adui huyo.