Na Amiri Kilagalila, Njombe.
Vijana zaidi ya 200 mkoani Njombe kutoka idara za Bodaboda, Bajaji, Mama na Baba lishe pamoja na idara ya Senet wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu wamejitokeza ofisi ya CCM mkoa kwa lengo la kujaza fomu ya kumdhamini mgombea Urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt,John Pombe Magufuli.
Katibu wa jumuiya ya vijana UVCCM mkoa wa Njombe Ndg,Amosi Kusakula amesema mara baada ya Mgombea nafasi ya Urais kupitia CCM Dkt, John Magufuli kuchukua fomu na kutangaza kutafuta Wadhamini kwenye mikoa yote, Mkoani Njombe vijana hao wamejitokeza na kutangaza kumdhamini Mhe,Magufuli ili arudi kwa awamu ya pili kuwatumikia watanzania.
Baadhi ya vijana hao akiwemo Bw, Seleman Matimbwi, Bi, Dorice Mwairubi na Bw, Fedrick Kaberege Wamesema kutokana na kazi kubwa aliyoifanya Dkt,Magufuli akiwa Madarakani imetosha wao na Wananchi kumshukuru na kumdhamini ili arudi kuwatumikia tena Watanzania kwa miaka mitano ijayo.
“Tumeona mambo makubwa ambayo Rais wetu ameyafanya akiwa madarakani ndio maana tupo hapa kwaajili ya kumdhamini ili arudi Ikulu kwa awamu ya pili tayari kwaajili ya kuwatumikia Watanzania” Wamesema vijana hao.
Bw, Norberth Kindole katibu wa umoja wa Madereva Pikipiki maarufu kama Bodaboda mkoa wa Njombe amesema kupitia umoja wao wameamua kujiunga kwa kauli moja kujitokeza kwenye ofisi za CCM mkoa wa Njombe ili kumdhamini Dkt, Magufuli.