F TAKUKURU Bagamoyo yawapa somo wanafunzi wa vyuo | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

TAKUKURU Bagamoyo yawapa somo wanafunzi wa vyuo


Na Omary Mngindo, Bagamoyo

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, imewataka wanafunzi wa vyuo kutokubali kujiingiza katika vitendo vyovyote vinavyohusiana na rushwa ikiwemo ya ngono.

Hali hiyo inayodaiwa kuwepo katika baadhi ya vyuo hapa nchini, inachangiwa na walimu wasiozingatia maadili ya kazi zao, kwa upande wa pili baadhi ya wanafunzi wachache wasio na uwezo darasani, kuwashawishi Waadhili wawapatie upendeleo wa alama za juu.

Hayo yalielezwa na Mkuu wa Taasisi ya Sanaa ya Utamaduni wilayani Bagamoyo mkoani hapa (TASUBA) Dr. Herbert Makoye, akitoa mada kwenye kongamano la rushwa ya ngono likihudhuliwa na Meneja wa Takukuru Mkoa Suzan Raymondi na wakuu wa vyuo mbalimbi wilayani hapa.

"Utamkuta Mhadhili ana miaka 60 au 30 anamtaka mwanafunzi wa miaka 20, akikataa ajiandae kupata ufaulu wa chini ama kufeli kabisa, wakati mwingine tamkuta mwanafunzi alikosa mkopo, familia ikakuuza mali, wengine vitu vya nyumbani ili aende chuo anajikuta anaingia mtegoni, ili amalize aende kusaidia familia," alisema Makoye.

Aliongeza kuwa zipo taarifa za baadhi ya wanafunzi wa kike vyuoni kulalamikiwa kutumia vibaya jinsia zao, kwa kuwatega Waadhili wa kiume kwa lengo la kuwapatia alama nzuri za masomo, hiyo inatokana na uwezo mdogo wa kimasomo darasani, hali ambayo pia inachangiwa na mwanafunzi kutojiheshimu.

Kwa upande wake Suzan alisema kuwa rushwa ya ngono haipo vyuoni tu hata katika siasa ikiwemo sehemu za kazi, ambapo kuna watu wanaopandishwa vyeo kwenye maofisi na kwamba chanzo kimojawapo ni mmomonyoko wa maadili, hivyo wanatakiwa kukabiliana na changamoto hiyo.

"Shughuli zetu TAKUKURU imeainishwa katika kifungu cha 7 cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007, ukiipata hiyo sheria utaona majukumu yetu, kati ya hayo mojawapo kushirikiana na wadau mbalimbali katika kupambana na rushwa ndio maana leo tupo hapa," alisema Suzan.

Aliongeza kwamba katika kutekeleza jukumu hilo, TAKUKURU imeingia makubaliano na shirika lisilo la kiserikali la Womain Fund Tanzania (WFT), kuhakikisha wanashughulikia kero ya rushwa ya ngono nchini, ambalo limesaidia kwa kiwango kikubwa kukabiliana na tatizo hilo, kwa kuwapatia elimu wadau mbalimbali.

Kwa upande wake Profesa Ralph Masenge kutoka Maruco alisema kuwa rushwa ni malipo ya aina yeyote yasiyo rasmi, ambayo hutolewa na mtu mwenye uhitaji, huku ikipokelewa na mtoa huduma husika kama mojawapo la sharti, ambalo inaweza ikawa haki yake au la.

Mmoja wa washiriki ameihoji taasisi hiyo namna inavyoweza kabiliana na rushwa ya ngono, ambayo inafanyika kwa usiri mkubwa, ambapo ofisa wa TAKUKURU aliijibu kwa kueleza kwamba kesi zinazofanana na hiyo nyingi wamezifanyiakazi, na kwamba baadhi ya wahusika wamekumbana na mkono wa sheria kuhusiana na vitendo hivyo.

Kongamano hilo lililohudhuliwa pia na Mkuu wa Takukuru wilaya ya Bagamoyo Christine Temba, limeshirikisha baadhi ya vyuo vikiwemo vya Ukutubi kinachofundisha Manesi cha Muhimbili, Tasuba, Adem na Kaole likiwa na kaulimbiu ya Mwanafunzi kataa rushwa ya ngono.