F Wanunuzi wa ufuta Lindi Mwambao watakiwa kuzingitia masharti | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Wanunuzi wa ufuta Lindi Mwambao watakiwa kuzingitia masharti



Na Ahmad Mmow, Lindi.

Kampuni zilizofanikiwa kununua ufuta  katika mnada wa kwanza katika chama kikuu cha ushirika cha Lindi Mwambao wamekumbushwa kuzingatia masharti ili kuepuka usumbufu usio walazima.

Wito huo umetolewa leo mjini Lindi na meneja mkuu wa chama hicho, Nurdiin Swallah alipozungumza na Muungwana Blog kwenye ofisi kuu ya chama hicho.

Swallah ambaye chama chake kilifanya mnada wakwanza tarehe 6.6.2020 katika mtaa wa Ng'apa, manispaa ya Lindi alisema wafanyabiashara, hasa kampuni tano zilizofanikiwa kununua  katika mnada huo zinatakiwa kutekeleza masharti ili kuepuka usumbufu usio wa lazima na malalamiko toka kwa wakulima.

Meneja huyo ambaye chama chake kilifanikiwa kuuza kilo 2,420,886 katika mnada huo alisema miongoni mwa masharti muhimu ni kampuni kuondoa ufuta ndani ya siku saba kwenye maghala ya chama hicho tangu siku ziliposhinda minada na kununua.

Alisema kwakufanya hivyo zitakuwa zimetoa nafasi kwa maghala hayo kuhifadhia ufuta wawakulima ambao utauzwa katika mnada ujao unaotarajiwa kufanyika tarehe 13.6.2020 katika mtaa wa Tulieni, manispaa ya Lindi.

Kwahiyo watakuwa wameepusha malalamiko,  wakulima  watauuza ufuta wao badala ya kushindwa kutokana na kushindwa kuhifadhiwa kwenye maghala hayo.

Swallah alizikumbusha kampuni kulipa haraka fedha za wakulima. Kwani miongoni mwasababu zinasababisha malalamiko kwa vyama vikuu na serikali kutoka kwa wakulima ni baadhi ya kampuni kuchelewesha fedha za malipo ya wakulima.

 '' Kuchelewa kutoa mzigo na kuingiza fedha kwenye akaunti ni kukiuka masharti nikinyume cha sheria. Sasa nimuhimu watekeleze hayo ili kusiwe na lawama wala malalamiko kutoka kwa wakulima,'' alisisitiza Swallah.

Kuhusu utaratibu wa malipo ya fedha za wakulima, alisema wanunuzi wataingiza fedha kwenye akaunti ya chama kikuu hicho, ambacho kitapeleka benki ambayo itaingiza moja kwa moja kwenye akaunti za wakulima.

Mtendaji mkuu huyo wa Lindi Mwambao aliwatoa hofu wakulima kuhusu changamoto ya vifungashio.

Alisema chama hicho kimejipanga vizuri,  hakutakuwa na changamoto hiyo na tayari kimesambaza viloba 296,000 katika vyama vyake vya msingi(AMCOS).

Katika mnada wa kwanza kampuni kumi zilijitokeza kununua. Hata hivyo nikampuni tano zilifanikiwa kushinda zabuni na kununua.

Ambapo ufuta ulinunuliwa bei ya juu ya  shilingi 2,112 na bei ya chini ni shilingi 2,053 kwakila kilo moja.

Kampuni zilizo fanikiwa kuuziwa na kununua ufuta kwenye mnada huo wa kwanza ni Afrisian Ginning Ltd, Mohamed Enterprises Ltd, Export Trading Ltd, RBST International Ltd na Yi hai kerry Hyseas.