F Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero yawakaribisha wadau kushiriki katika uhifadhi misitu, mazingira | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero yawakaribisha wadau kushiriki katika uhifadhi misitu, mazingira

 MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro Hassan Njama amewakaribisha wadau wa uhifadhi wa mazingira kushiriki kikamilifu uhifadhi wa misitu na utunzaji mazingira huku akitumia nafasi hiyo kusisitiza umuhimu wa utoaji elimu kwa wananchi kuhusu Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ).


Pamoja na kuwepo kwa wadau mbalimbali, amesema amevutiwa na jitihada zinazofanywa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Jamii Tanzania (TFCG) pamoja na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) ambao kwa wamekuwa wakishirikiana na wananchi na viongozi wa wilaya hiyo kukabiliana na channgamoto zilizopo katika uhifadhi wa misitu.


Akizungumza na waandishi wa habari nchini pamoja na baadhi ya maofisa kutoka TFCG na MJUMITA waliofika ofisini kwake kwa ajili ya kupata maelezo kuhusu namna ambavyo Wilaya hiyo imekuwa ikishirkiana na wadau hao katika kuhifadhi misitu, Njama ametumia nafasi hiyo kufungua milango kwa wadau hao na wengine akimiani kuwa ili kuendeleza uhifadhi wa misitu na utunzaji wa mazingira inahitaji ushirikiano wa kila mmoja wetu.


Amesema ni vema wadau wa uhifadhi wa mazingira mkatambua milango iko wazi na watashirikiana kwa mjibu wa ratatibu, kanuni na sheria mbalimbali zilizopo ambazo zinahusu nafasi ya wadau kushiriki katika uhifadhi wa misitu."MJUMITA na TFCG , hakika mmefanya kazi kubwa sana kupitia mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS)ambao unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Uswis (SDC).


"Katika Wilaya yetu hii ya Mvomero, vijiji vyetu 10 vimenufaika na uwepo wenu kupitia mradi wenu ambao umejikita katika kuleta mageuzi katika sekta ya mkaa. Kumekuwepo na mradi maarufu sana wa mkaa endelevu na faida yake tumeiona , wananchi ambao wamekuwa na mradi huo wamepiga hatua kubwa kimaendeleo.


"Malengo yetu halmashauri ya Wilaya ya Mvomero tunataka kuongeza vijiji vingine 10 ambavyo vitakuwa na mradi huo wa mkaa endelevu na utoaji elimu sahihi kuhusu uhifadhi wa misitu.


Tunaamini katika bejeti ya fedha ya mwaka huu tutaanza kutekeleza mpango huo,"amesema Njama.

Hata hivyo amefafanua wataendelea kutoa elimu kwa wanavijiji ambao wanamiliki misitu ya vijiji pamoja na viongozi ili kila mmoja awe balozi wa USMJ huku akisisitiza USMJ katika wilaya yao itatekelezeka kwa urahisi kwani vijiji 101 kati vijiji 167 vinampango wa mpango wa matumizi bora ya ardhi.


Wakati huo huo amesema tangu ameingia katika ofisi hiyo mwezi mmoja uliopita baada ya kuteuliwa kushika nafasi huyo, changamoto kubwa ambayo ameiona ni migogoro ya ardhi kwani tayari ameshapokea kesi 21, hivyo kupitia mikakati ya wilaya hiyo itasimama imara kutafuta ufumbuzi

wa kudumu.


Akizungumza mbele ya Mkurugenzi huyo, Ofisa Sera na Majadiliono kutoka MJUMITA Elida Fundi ametumia nafasi hiyo kueleza yale ambayo wamekuwa wakiyafanya kwa kushiririkiana na wananchi wa Mvomero na kwamba wao wamejikita zaidi kwenye USMJ ili rasilimali misitu na mazingira yawe salama.


"Mradi huu wa TTCS umemalizika Novemba mwaka 2019, hata hivyo tumekuja na mradi mwingine ambao wenyewe utajikita kutoa mafunzo kwa ngazi zote.Hata hivyo kwa minne nane tumekuwa tukitekeleza mradi wa TTCS.


"Hivi sasa tumekuja na Mradi wa Kuhifadhi, Misitu kwa Kuwezesha Biashara Endelevu ya Mazao ya Misitu Tanzania (CoForEST).Tunaomba Mkurugenzi tuendelee kushirikiana kama ambavyo tumekuwa tukishirikiana wakati wote kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo,"amesema Fundi.


Ofisa Misitu Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro Edward Kimweri ameeleza kuwa misitu ndani ya wilaya hiyo iko salama kwani wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa kutunza misitu na mazingira na kwamba mradi wa TTCS umechochea maendeleo na uhifadhi kwa kiwango kikubwa.


"Tumekuwa na utaratibu mzuri wa kulinda na kuhifadhi misitu yetu katika Wilaya yetu ya Mvomero.Tutaendelea kuweka mipango madhubuti kutunza misitu na mazingira yanayotuzunguka.Tunafahamu jamii iliyozungukwa na misitu ya asili imekuwa mfano wa kuigwa katika kuilinda na hiyo inatokana na kuona faida kubwa ambayo inapatikana,"amesema.


Kuhusu tangazo la Serikali GN 417, Kimweri amesema kwamba mtazamo wake anaona ina faida na hasara, hivyo kinachotakiwa ni watu wote wajipange kukabiliana nayo kwa maslahi ya misitu.


Kwa upande wake Ofisa Sera na Majadiliono kutoka MJUMITA, Elida Fundi alimueleza sababu ya wao kujikita katika USMJ ni kuhakikisha rasilimali misitu na mazingira yanakuwa salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo.


Amesema mradi wa TTCS umefikia kikomo Novemba 2019 lakini wamekuja na mradi mwingine ambao utajikita katika mafunzo kwa ngazi zote.


"Kwa takribani miaka nane tumekuwa tukitekeleza mradi wa TTCS,kwa sasa tumekuja na Mradi wa Kuhifadhi, Misitu kwa Kuwezesha Biashara Endelevu ya Mazao ya Misitu Tanzania (CoForEST) ni imani yangu tutaenda pamoja ili misitu yetu iwe salama na endelevu," alisema.

Post a Comment

0 Comments