F Mgombea Ubunge Jimbo la Njombe mjini Deo Mwanyika akabidhiwa fomu | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Mgombea Ubunge Jimbo la Njombe mjini Deo Mwanyika akabidhiwa fomu



Na Amiri Kilagalila,Njombe

Mgombea Ubunge wa jimbo la Njombe Mjini kupitia chama cha mapiduzi CCM Deodatus Mwanyika amesema sera yake ya dira mpya na Njombe mpya itakwenda kuwa muarobaini kwa maendeleo ya jimbo hilo huku akimshukuru rais magufuli na chama cha mapinduzi kwa kumuamini na kumteua kwenda kupeperusha bendera ya ccm katika nafasi ya ubunge.

Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na vyombo vya habari baada ya kuchukua fomu kwa msimamizi wa uchaguzi jimbo la njombe mjini kwa ajili ya kwenda kushindani na vyama vingine vya upinzani kuelekea katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika oktoba 28 mwaka huu.

“Nimshukuru mwenyekiti wa Chama Taifa,kamati kuu na halmashauri kuu ya CCM kwa kuniamini lakini niwashukuru vile vile wapiga kura wa Njombe kwasababu wao vile vile wameonesha nia kwangu,lakini leo kwa mara ya kwanza tumekwenda kuchukua fomu ya tume ya Uchaguzi ili tuweze kutambulika rasmi”alisema Mwanyika.


Kwa upande wake msimamizi wa uchaguzi jimbo la Njombe mjini ambaye ni mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Njombe Iluminata Mwenda amewataka wagombea wote waliofika kuchukua fomu hizo kwenda kuzijaza kwa ufasaha na kwa usahihi mkubwa kwa mujibu wa maelekezo ya tume ya uchaguzi.

“Wagombea wanatakiwa kuzijaza kwa usahihi,wapate wadhamini lakini pia waandike majina yao yaweze kuonekana”alisema Iluminatha Mwenda

Vyama vinne vya CCM,Chadema,Chauma na ACT wazalendo tayari vimeshawapeleka wagombea wao wa ubunge kuchukua fomu za kwa ajili ya kupeperusha bendera ya vyama katika uchaguzi mkuu ujao ngazi ya Jimbo.