Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuanza kuwakatia umeme wateja wake wenye madeni sugu nchi nzima, ifikapo Agosti 31, mwaka huu.
Alitoa maelekezo hayo akiwa katika ziara ya kazi wilayani Siha, Mkoa wa Kilimanjaro, Agosti 17, 2020 kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme ambapo pia aliwasha umeme katika taasisi za umma na makazi ya wananchi.
Alisema TANESCO inadai zaidi ya shilingi bilioni 300 kutoka kwa Mashirika hasa ya Umma, Halmashauri, Sekta ya Afya, Mambo ya Ndani, Maji, Ulinzi na nyingine nyingi.
“Natoa siku 14 kuanzia sasa kwa Taasisi zote zinazodaiwa zikiwemo za Umma, zilipe, zisipolipa tutakata umeme, tena bila huruma wala taarifa nyingine yoyote. Taarifa ndiyo hii,” alisisitiza.
Akielezea sababu za kufikia uamuzi huo, Waziri Kalemani alisema Shirika hilo linajiendesha kibiashara pasipo kupata ruzuku serikalini, hivyo malimbikizo ya madeni ya wateja yanahatarisha uhai wake.
Alieleza baadhi ya miradi inayoendelea kutekelezwa na Shirika hilo kwa kutumia fedha za ndani kuwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kupeleka gridi ya Taifa mkoani Kigoma pamoja na kusambaza miundombinu mingine katika vijiji na mitaa kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
“Kwahiyo ni lazima tuwe na vyanzo vya uhakika vya ndani ambavyo pamoja na mambo mengine, ni kwa wateja wetu kutulipa kwa wakati.”
Aidha, Dkt Kalemani alitahadharisha kuwa wakati wa utekelezaji wa suala hilo, asipigiwe simu na wadaiwa zenye mlengo wa kumsihi kusitisha kutokana na sababu ambayo hutolewa na wengi kuwa taasisi zao ni muhimu hivyo zisikatiwe umeme. Alisisitiza kuwa badala ya kupiga simu, wadaiwa walipe ankara zao.
Katika hatua nyingine, akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, Waziri alimweleza kuwa Mkoa huo una umeme mwingi ikilinganishwa na mahitaji yake.
Alisema kuwa Mkoa una zaidi ya megawati 110 za umeme wakati matumizi yake ni megawati 45 hadi 48, hali inayoufanya kuwa na ziada kubwa kuliko mahitaji.
Aidha, alieleza kuwa kwa sasa Serikali kupitia Wizara yake, inafuatilia utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini inayoendelea, ambayo ni REA II na REA III.
Alisema ameunda kikosi kazi maalumu kinachojumuisha wataalamu kutoka wizarani, TANESCO Makao Makuu na REA Makao Makuu, kitakachowajibika kuhakikisha Miradi hiyo ya umeme inakamilika ifikapo Septemba 15, 2020.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa alipongeza kazi kubwa inayofanywa na Wizara lakini akaomba kusimikwa kwa nguzo za umeme zilizo imara zaidi, hususan katika maeneo ya milima ambako kuna upepo mkali, ili ziweze kuhimili hali hiyo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Siha, Onesmo Buswelu, alisema Wilaya yake ina deni kwa Rais John Magufuli ambalo inawiwa kulilipa kutokana na kuwajali wananchi hao kwa kuendelea kuwapigania katika nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo umeme.
Katika ziara hiyo, Waziri alifuatana na Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Dkt Tito Mwinuka, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga pamoja na Wataalamu wengine mbalimbali kutoka Wizarani na katika Taasisi hizo.
0 Comments