F Mkongo wa Taifa wa mawasiliano waunganisha visiwa vya Pemba na Unguja | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Mkongo wa Taifa wa mawasiliano waunganisha visiwa vya Pemba na Unguja

 


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeweka saini ya mkataba wa makubaliano wa kuunganisha visiwa vya Pemba na Unguja na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Mkongo wa Zanzibar

Utiaji saini huo umeshuhudiwa na katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Zainabu Chaula wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dkt. Mustafa Aboud Jumbe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

Utiaji saini huo umefanywa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Waziri Kindamba kwa upande wa Bara na Mhandisi Shukuru Awadh Slueiman, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Miundombinu ya TEHAMA Zanzibar (ZICTIA) kwa upande wa Zanzibar


Kabla ya kushudia tukio hilo, Dkt. Zainabu Chaula alisema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 700 na kuunganisha kwenye mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na kwenye nchi jirani za Congo, Zambia, Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda na Malawi ambapo maunganisho haya yanaenda kufungua fursa za wawekezaji na watumia wa huduma za mawasiliano wa ndani na nje ya nchi kuunganishwa na Zanzibar kwa kuwa katika kipindi cha miaka mitano tumeshuhudia kuibuka kwa mifumo ya TEHAMA ambayo inawezesha utoaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi kwa kasi zaidi


Naye Dkt. Jumbe amesema kuwa haya ndio matunda ya mapinduzi, matunda ya mapinduzi sio maembe wala mapapai bali ni maendeleo yanayopatikana katika nchi yetu, na Serikali yetu ya SMZ imetumia zaidi ya shilingi bilioni 30 kuunganisha mikoa na wilaya zote za Unguja na Pemba bali kulikuwa na changamoto ya kuunganisha Unguja na Pemba ila sasa kwa kupitia makubaliano haya, tutatumia barabara ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kuunganisha visiwa Pemba na Unguja na hivyo Zanzibar kuunganishwa na Tanzania Bara moja kwa moja na utawezesha kupunguza gharama za mawasiliano ili ziwe nafuu

Ndugu Kindamba amesema kuwa ufunguzi wa njia za mawasiliano ya Mkongo kati ya Tanzania Bara na Zanzibar utakuwa na manufaa makubwa sana kwa taifa hasa katika kuwezesha kuongezeka kwa matumizi ya data na intaneti na makubaliano hayo yanahusisha kutunza vifaa vya miundombinu ya TEHAMA vya ZICTIA kwenye majengo ya TTCL

Mhandisi Suleimani ameongeza kuwa ZICTIA imekamilisha ujenzi wa Mkongo wa Zanzibar na sasa unaunganishwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambapo itakuza na kuongeza huduma za mawasiliano; kuondoa changamoto iliyokuwepo Zanzibar ya kutumia njia ya mawasiliano ya mawimbi ya radio kutoa huduma za mawasiliano ambayo hayana kasi na ubora unaohitajika, kupunguza gharama za mawasiliano na kuingizia mapato kwa Serikali

Post a Comment

0 Comments