Wanamgambo wanaoshukiwa kuwa wa makundi ya itikadi kali, wamewauwa takriban watu 11 Kaskazini Mashariki mwa Nigeria wakati wa shambulizi dhidi ya msafara wa maafisa wa usalama uliokuwa ukiwarejesha makwao watu waliopoteza makazi yao kutokana na uasi.
Duru za polisi zimesema haya hapo jana.Kupitia shirika lake la habari la Amaq, kundi la wanamgambo linalojiita Dola la Kiislamu IS limesema kuwa maafisa 30 wa polisi na wanajeshi waliuawa katika shambulizi hilo la Ijumaa katika barabara inayoelekea katika mji wa Baga wenye shughuli nyingi za uvuvi katika jimbo la Borno.
Katika taarifa hapo jana, idara ya polisi ya jimbo la Borno ilisema kuwa maafisa wanane wa polisi na wanajeshi watatu wa serikali waliuawa na watu 13 kujeruhiwa katika shambulizi hilo.
Wanamgambo wa kundi hilo la IS wamewasababishia zaidi ya watu milioni 2 kutoroka makazi yao tangu mwaka 2009 wakati kundi la uasi la Boko Haram lilipoanza uasi unaolenga kuanzishwa kwa taifa linalozingatia sheria za kiislamu. Takriban watu elfu 30 wameuawa katika ghasia hizo.
0 Comments