Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maji yenye thamani ya shilingi bilioni 49.7 kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kigoma (KUWASA).
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma na Ufuatiliaji wa Wizara ya Maji Mhandisi Lyidia Joseph.
Amesema hayo kwa niaba ya Mhandisi Sanga wakati akizindua bodi mpya ya muhula wa saba ya KUWASA baada ya ile ya awali iliyoanza kazi mwezi Julai 2016 muda wake kukamilika Juni 2019.
Akizindua bodi hiyo mpya Mhandisi Lyidia amesema zipo changamoto zinazohitaji utatuzi hivyo kuitaka bodi mpya kujipanga na kuendeleza jitihada zilizofikiwa na bodi iliyopita na kuhakikisha misingi ya uendeshaji wa mamlaka inaimarika.
Amesema Serikali imejipanga kumaliza changamoto ya huduma ya maji mkoani Kigoma ambapo ipo miradi inayotarajiwa kuanza itakayogharimu kiasi cha shilingi bilioni 9.8, ikiwamo ujenzi wa kitekeo kipya cha maji katika eneo la ufukwe la Amani, ukarabati wa miundombinu ya mradi wa maji Mwandiga na mradi wa uondoaji majitaka Manispaa ya Kigoma.
Bodi mpya ya KUWASA imetakiwa kutumia nyenzo iliyokabidhiwa kuwa kichocheo katika kurahisisha utekelezaji wa majukumu, ikiwemo Sheria ya Maji Na. 5 ya mwaka 2019, na Mpango wa Biashara wa Mamlaka kwa mwaka 2019/2020-2021.
0 Comments