Polisi nchini Belarus sasa wataruhusiwa kutumia silaha za kivita mitaani kama kutakuwa na haja ya kufanya hivyo ili kukabiliana na kile wizara ya mambo ya ndani imeelezea kuwa ni kuongezeka kwa maandamano makubwa ya msimamo mkali dhidi ya serikali.
Wizara hiyo imesema maandamano hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yamehamia katika mji mkuu Minsk, yamekuwa ya kupangwa na ya hisia kali.
Polisi imesema imewakamata watu 713 katika maandamano ya jana ambapo vikosi vya usalama vilitumia mizinga ya maji na virungu kuyavunja makundi yanayodai uchaguzi mpya wa rais.
Maelfu ya Wabelarus wameandamana kila mwisho wa wiki tangu uchaguzi wa Agosti 9 ambao Rais Alexander Lukashenko alitangazwa mshindi.
Wapinzani wake wanadai matokeo yalichakachuliwa, Lukashenko anakanusha kuiba kura. Viongozi wengi wa upinzani wamekimbia nchini au kukamatwa.
0 Comments