F Kupanda, kushuka waliofukuzwa Chadema | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Kupanda, kushuka waliofukuzwa Chadema


Kama sakata hili litaishia kupoteza ubunge wa viti maalum, itakuwa ni mwenendo wa kupanda na kushuka kwa makada 19 waliovuliwa uanachama wa Chadema Ijumaa baada ya kukaidi msimamo na chama hicho na kwenda Dodoma kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum.


Waliovuliwa uanachama ni Halima Mdee, Ester Bulaya, Grace Tendega, Nusrat Hanje, Hawa Mwaifunga, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Salome Makamba na Jesca Kishoa.


Wengine ni Tunza Malapo, Kunti Majala, Anatropia Theonest, Conchesta Rwamlaza, Cecilia Pareso, Agnesta Lambert, Asia Mohammed, Stella Fiao na Felister Njau.


Akitangaza maazimio ya Kamati Kuu, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema wajumbe waliazimia kw akauli moja kuwavua uanachama makada hao baada ya kukiuka kanuni za chama hicho kwa uamuzi wao wa kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum.


Mbowe alisema wabunge hao walikwenda kuapishwa bila kupitishwa na kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho, jambo lililosababisha sintofahamu ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini.


Makada hao, ambao pia hawakujitokeza mbnele ya Kamati Kuu kuhojiwa wana histyoria na rekodi tofauti.


Mdee, mwenyekiti wa wanawake

Anayeonekana zaidi katika kundi hilo ni Mdee, ambaye ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bavicha). Mdee aliingia kwa mara ya kwanza bungeni mwaka 2005 kwa tiketi ya viti maalumu. Alijipambanua kama mbunge mwenye msimamo katika masuala anayoyaamini, huku akionyesha uwezo wa kujenga hoja.


Mwaka 2010 aligombea ubunge wa Kawe na kushinda. Alifanikiwa kukalia kiti hicho hadi mwaka 2020 aliposhindwa na Askofu Josephat Gwajima wa CCM.


Mwaka 2014, Mdee aligombea uenyekiti wa Bawacha na kushinda kwa kishindo na kutetea nafasi hiyo mwaka 2019.


Ushindi wa kura, mahakamani

Kada mwingine anayeonekana sana ni Bulaya, ambaye aliingia bungeni 2010 kwa viti maalum vya CCM, lakini alihamia Chadema mwaka 2015 na kugombea ubunge wa Bunda, ambako alimshinda mwanasiasa mkongwe wa CCM, Steven Wassira.


Baada ya Tundu Lissu kushambuliwa kwa risasi na kwenda nje ya nchi kwa matibabu, Mbowe alimteua Bulaya kuwa mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni (KUB).


Bulaya, ambaye alitokea Umoja wa Vijana wa CCM, pia alikuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu, Kamati Kuu na Mkutano Mkuu.


Mtendaji wa Bawacha

Tendega anaweza kuwa kada mwingine kigogo katika orodha ya waliotimuliwa. Alikuwa katibu mkuu wa Bawacha. Alianza kugombea ubunge uchaguzi mdogo wa Kalenga mwaka 2013 lakini hakushinda.


Lakini mwaka 2014 alichaguliwa kuwa katibu mkuu wa Bawacha na mwaka 2015 na 2020 aligombea nafasi ya ubunge wa jimbo hilo hilo, lakini hakufanikiwa.


Aliingia bungeni kwa mara kwanza mwaka 2015 akiwa mbunge wa viti maalumu.


Mpambanaji

Katika waliotimuliwa, yumo Matiko mwenye sifa ya upambanaji. Aliwahi kufanya kazi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na aliingia bungeni mwaka 2010, akiwa mbunge wa viti maalum, lakini mwaka 2015 aligombea jimbo la Tarime Mjini na kuibuka kidedea.


Pia aliwahi kuwa mweka hazina wa Bawacha pamoja na mwenyekiti wa Chadema kanda ya Serengeti na mjumbe wa Kamati Kuu.


Hanje

Kuchaguliwa na uapishwaji wake kuwa mbunge wa viti maalumu ulizua gumzo katika jamii, kwa kuwa yeye na wenzake walikuwa gerezani kwa miezi minne mkoani Singida. Alikuwa katibu mkuu wa Bavicha.


Mwaifunga

Ni makamu mwenyekiti wa Bawacha Bara ambaye aliingia bungeni mwaka 2015 akiwa mbunge wa viti maalum na mwaka 2020 aligombea ubunge wa Tabora Mjini na kushindwa.


Aliteuliwa kuwa makamu mwenyekiti wa baraza hilo mwaka 2014, lakini mwaka 2019 alifanikiwa kutetea nafasi kwa mara nyingine.


Kaboyoka

Alijizolea umaarufu tangu mwaka 2015 baada ya kumshinda mpinzani wake, Anne Kilango Malecela wa CCM katika jimbo la Same Mashariki mkoani Kilimanjaro. Baada ya kuingia Bungeni aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).


Katika nafasi ya uenyekiti wa PAC Kaboyoka anatajwa kufanya vizuri katika kipindi chake chote alichohudumu katika nafasi hiyo.


Kishoa

Alikuwa mgombea ubunge wa Iramba Magharibi mwaka 2015 hadi 2020 lakini hakufanikiwa. Mwaka 2015 aliteuliwa kuwa mbunge wa viti maalum.


Mwaka 2019 aliteuliwa kuwa Naibu katibu mkuu wa Bawacha Bara akimshinda mshindani wake Kunti Majala aliyekuwa akiitetea nafasi hiyo.


Anatropia

Alikuwa mbunge wa viti maalumu mwaka 2015, aligombea ubunge wa Segerea mwaka huo lakini hakufanikiwa na mwaka kuu alikwenda kugombea jimbo la Kyerwa mkoani Kagera.


Makamba

Aliingia bungeni mwaka 2015 na mwaka huu aligombea ubunge jimbo la Shinyanga Mjini lakini alishindwa mbele ya mgombea wa CCM Patrobas Katambi.


Ni miongoni mwa wabunge waliong’ara katika Bunge la 11 kwa namna alivyokuwa akiwasilisha hoja na hotuba mbadala za kambi ramsi ya upinzani Bungeni.


Alichokisema Mbowe

Juzi saa 5:00 usiku Mbowe alitangaza uamuzi wa Kamati Kuu ya kuwavua uanachama makada hao.


Mbowe alisema Mdee na wenzake waliitwa kwa barua, lakini hawakutokea.


“Dada zetu, nini kimetokea? Tumewaita tena kwa barua, lakini wote kwa pamoja waliomba kuongezewa muda wa kuja Kamati Kuu,” alisema Mbowe.


“Tumewaita waje dada zetu na ndugu zetu wanasema hawawezi kuja wakisema wanaomba kuongezewa muda wa wiki moja ili watafakari tuhuma zao kwa maslahi ya chama hiki. Unapewa nafasi ya kuja kujitetea uamuzi wako unaomba upewe muda wa kutafakari mbona hakutafakari wakati wa kuapa?”


Mbowe alisema ofisi ya katibu mkuu iliandika barua nyingine ikiwataka waende kwa ajili ya kujieleza, lakini wote kwa umoja hawakutokea, kitu alichosema ni kufanya ujeuri.


“Tumejitahidi kadri ya uwezo wetu ikiwemo kuwapigia simu tukiwataka waje ili kutengeneza amani na Chadema, lakini hawakuja,” alisema.


Mbowe alisema kwa mujibu wa kifungu cha 6 pointi 5 na moja ( b), Kamati Kuu imeazimia kuwavua uanachama wanachama wake wote 19 waliokula kiapo Novemba 24 ili kuwa wabunge wa viti maalum


“Hiki chama kinapitia maumivu makubwa. Hawa dada zetu wamekuwa sehemu ya mapambano, sijui nini kimewakumba?” alisema Mbowe.


Alisema alisema “maumivu yake hayaelezeki kwa maneno. Hatufanyi maamuzi kwa kushangilia bali tunafanya kwa maumivu makubwa”.


Alisema baada ya kutafakari kwa kina wajumbe waliazimia masuala mbalimbali, likiwemo la kuwavua nyadhifa zao zote za uongozi ndani ya Chadema kwa kuwa hawana sifa za kuendelea na nafasi hizo.


“Wanatakiwa wasijihusishe kwa namna yoyote na shughuli zozote zinazohusu Chadema kuanzia dakika hii ninavyozungumza. Tunaelekeza kamati tendaji za Bawacha na Bavicha kuziba nafasi za viongozi hao,” alisema.


Kwa mujibu wa Mbowe, viongozi sita wa Bawacha kuanzia mwenyekiti na makamu wake bara, katibu mkuu na manaibu wake wa Zanzibar na bara na mwenezi wao walishiriki mchakato huo aliouita ni uasi ndani ya chama hicho.


Mbowe pia alisema kiapo chao ni batili, ndiyo maana wajumbe wa Kamati Kuu wameilekeza kurugenzi ya sheria ya chama hicho kufuata utaratibu wa kisheria kuupinga mchakato huo.


“Chama hakijapeleka watu, wameghushi majina na wao wameyapokea. Yaani wabunge wetu wanakwenda kuratibiwa na…Hatuwezi kukubali mambo haya,” alisema Mbowe.


Hata hivyo, katika barua yake ya juzi mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk Wilson Mahera alisema katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika alimuandikia barua Novemba 19 yenye orodha ya majina ya wanachama 19 waliopendekezwa kuwa wabunge wa viti maalum na tume ilitumia barua hiyo kuwateua.


Chadema, iliyopata mbunge mmoja tu, inastahili nafasi 19 za ubunge wa viti maalum kutokana na kupata idadi ya kura za wabunge zinazozidi asilimia 5, kiwango ambacho hutumiwa kuanzia kutoa nafasi hizo kwa vyama.

Post a Comment

0 Comments