Ali Hussein Kadhim, ni mwanajeshi wa Iraq na Muislamu wa dhehebu la Shia, alitekwa katika mji wa Tikrit na waliofahamika kama wanamgambo wa kundi la Islamic State June 2014.
Miaka mitatu baada ya vikosi vya Marekani kujiondoa Iraq, nchi hiyo ikaingia vita upya mwaka 2014.
Ali Hussein, anakumbuka yaliyomtokea yeye pamoja na Waislamu wa dhehebu la Shia katika mji uliokuwa na nguvu wa Tikrit nchini Iraq, Juni 2014.
Fuatilia simulizi ya Ali Hussein.
Juni 24, 2014, wanamgambo wa Islamic State (IS) walitekeleza mauaji ya mamia ya vijana wadogo ambao walikuwa ndio wamejiunga na jeshi la Iraq na wakati huo walikuwa katika kambi ya mazoezi ya Speicher nchini humo kupata mafunzo.
"Ninapojiangalia nakumbuka kila kitu. Nakumbuka jinsi Mungu alivyoninusuru miongoni mwa watu wote waliouawa," Hussein amesema.
"Nilijiunga na jeshi la Iraqi kwasababu ya matatizo yangu ya kifedha. Hakuna kazi nyingine ambayo ningeweza kufanya kusaidia familia yangu," anasema.
Hussein anaishi katika mji wa Diwaniyah, kusini mwa mji wa Baghdad. Idadi kubwa ya watu huko ni wa dhehebu la Shia.
Kabla ya kutokea kwa shambulio la IS, Hussein alianza kufanya mazoezi katika kambi la Speicher kama mwanajeshi.
"Rafiki zangu na familia waliniambia, 'Usiende katika kambi ya Speicher kwasababu ni eneo la Tikrit, alikozaliwa Saddam Hussein. Wale waliotoa agizo la kuuawa kwa Saddam walikuwa Washia.'"
Siku za kwanza 12 kambini zilikuwa kawaida tu. Lakini ghafla mambo yakabadilika.
Kundi la IS liliwasili Tikrit na wanajeshi wengi waliokuwa kambini walivaa nguo za raia na kutoroka.
Lakini wakaacha maelfu ya wanajeshi wengi tu ambao hawakuwa wamepata mafunzo.
"Tulibadilisha nguo zetu za raia na kuondoka kambini tukiwa tunaonekana kama watu wa kawaida. Wanamgambo wa IS walikuja tulipokuwa na kusema: "Karibuni.", tuna silaha lakini hatutawadhuru."
"Musiogope, tunawapeleka tu katika makazi ya rais… "Mukisha apa kwamba hamutarejea tena jeshini, tunawaachilia," Hussein anasema hicho ndicho kilichotokea.
Baadhi ya viongozi wa IS walikuwa sehemu ya utawala wa Saddam Hussein.
Walipowasili katika makazi ya rais, wanajeshi wa dhehebu la Sunni wakaruhusiwa kwenda nyumbani lakini wanajeshi wa Shia akiwemo Ali Hussein wakamrishwa kulala chini.
"Nakumbuka vizuri kila kitu kilichotokea. Mmoja wa IS alituzungumzia kwa kelele, 'Tunalipiza kisasi kwa kile mulichokifanya kwa Saddam, tunawachinja', Nikasikia milio ya risasi."
Kisha wakasimamishwa na kupangwa mstari.
"Mwanamgambo mmoja wa kundi la IS alikuja kwenye mstari niliokuwa nimesimama na kuanza kutupiga risasi mmoja baada ya mwingine."
Walipompiga risasi mtu wa tatu karibu yangu damu yake ikanirukia mimi. Nikasikia risasi ya nne ambayo ilistahili kunipiga mimi, lakini sijui risasi hiyo ilikwenda wapi? Kila baada ya kumpiga mtu risasi mwanamgambo alikuwa anaupiga mwili wake teke," Hussein anazungumzia alichoshuhudia.
"Baada ya kupiga kila mmoja risasi mwanamgambo huyo alisimama kando kidogo. Lakini muda mfupi baadaye, mmoja wao akasema huyu bado anapumua, aliyekuwa anamzungumzia alikuwa mimi, kisha aliyekuwa amesimamia akasema, 'Achana naye "Huyo ni kafiri, ni wa dhehebu la Shia, muache asikie machungu na avuje damu hadi akutane na mauti yake.
Wakati huo, gaidi huyo hakujua kwamba Hussein hakuwa amepigwa risasi wala kuvuja damu. "Damu zilizokuwa zinanitiririka, zilikuwa za shahidi mwingine karibu nami."
"Nilisalia hapo hadi usiku wa manane. Nilikuwa na damu kila sehemu hadi masikioni. Sauti za wanaokufa, namna wanavyokata roho, zote nilizisikia mimi na sijui niliweza vipi kutulia kimya nikiwa na faamu zangu kipindi chote hicho."
"Namshukuru Mungu hatimaye nilifanikiwa kurejea kwa familia yangu, na siwezi kusahau nilichokiona - sio rahisi."
Wanajeshi 1,700 waliuawa na kundi la Islamic State. Hussein akiwa miongoni mwa wachache walionusurika mauaji hayo ya halaiki."
Hussein aliiambia BBC kwamba ilikuwa miujiza kwake kunusurika vita hivyo na kuwa hawahi kusahau kilichomtokea yeye pamoja na wanajeshi 1,700 waliokuwa wanapata mafunzo.
0 Comments