Na Omary Mngindo, Fukayosi
MBUNGE wa Jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani Miharami Mkenge, ameahidi kuchangia matofari elfu moja kwa ajili ya ujenzi wa zahanati katika Vitongoji vya Mwanavuli na Kalimeni Kata ya Fukayosi.
Mbali ya ahadi hiyo, pia ameanzisha harambee iliyofanikisha kupatikana kwa ahadi ya tofari 2,305 ambapo Kitongoji cha Mwanavuli alichangisha 950 ukiondolea ahadi yake, huku Kalimeni yakifikia 1,355 ukiweka kando atazozitoa yeye.
Hatua hiyo umetokana na wakazi katika Vitongoji hivyo kuelezea adha hiyo, inayowalazimu kutembea umbali mrefu kufuata huduma Makao Makuu ya Kata hiyo, au Kiwangwa hali inayowagharimu upande wa usafiri.
"Serikali yetu ya awamu ya Tano chini ya Rais wetu Dkt. John Magufuli imedhamiria kuwaondolea wananchi wetu changamoto mbalimbali, niwaombe sisi tuanze kuibua miradi tujichangishe kisha serikali itatuunga mkono," alisema Mkenge.
Aidha alielezea kufurahishwa kwake na mwamko aliouona kwa wakazi hao, huku akiwaagiza Wenyeviti wa vitongoji hivyo kuorodhesha nyumba kwa nyumba ili kila mkazi achangie juhudi hizo, zinazolenga kuwaondolea adha ya muda mrefu.
Kwa upande wake Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo John Fraansis "Bolizozo" alimtaka Kaimu Ofisa Mipango Omary Mshihiri kueleza lini vitongoji hivyo vitapata ramani za ujenzi wa zahanati hizo.
"Mwenyekiti na wasaidizi wake hawa wanataka kujua lini ramani ya ujenzi zitapatikana, sisi chama hatutapenda kuona wananchi hawa pamoja na kuwa na fedha zao, lakini mkawakwamisha katika ujenzi wai," alisema Fransis.
Akijibia hilo Mshihiri amesema kwamba ramani zinapatikana, huku akiwataka viongozi hao kufika haraka katika ofisi ya Halmashauri Bagamoyo kitengo cha ardhi wakachukue ramani hizo.
0 Comments