F Tanzania yapata mkopo wa bilioni 684.6 | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Tanzania yapata mkopo wa bilioni 684.6


Serikali za Tanzania na Korea zimetiliana saini mkataba wa mkopo wenye masharti nafuu wa Tsh Bil. 684.6, kupitia mfuko wa ushirikiano wa kiuchumi wa nchi hiyo kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi 5 ya maendeleo katika sekta za afya, maji, miundombinu na nishati.

Mkataba wa mkopo huo umesainiwa Jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James kwa upande wa Serikali na Balozi wa Korea hapa nchini Mhe. Cho Tae – Ick.

Akizungumza mara baada ya kutiliana saini hizi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James alisema kuwa mradi huo utahusisha ujenzi wa kituo cha kupooza umeme cha Kigoma cha msongo wa 400kv/132kv/33kv na upanuzi wa kituo cha kupooza umeme cha Nyakanazi cha msongo wa 400kv/220kv, utakao gharimu dola za Marekani milioni 45 sawa na shilingi bilioni 102.9

“Kukamilika kwa miradi hiyo kutaongeza umeme kupitia gridi ya Taifa na kupunguza changamoto ya upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Kaskazani Magharibi ya Tanzania na itapunguza gharama ya uendeshaji na ukarabati wa mitambo ya kuzalisha umeme unaotumia mafuta ya dizeli", amesema Katibu Mkuu James.

Aidha Katibu Mkuu amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Korea, imetoa mkopo wa dola za Marekani milioni 40 sawa na shilingi bilioni 91.4, kwa ajili ya kuboresha mfumo wa afya nchini kwa kuongeza uwezo wa kibajeti wa Serikali wa kukabiliana na madhara ya kibajeti yaliyotokana na ugonjwa wa Corona.

Aidha fedha hizo pia zitasaidia mradi wa uboreshaji wa huduma za majitaka katika Jiji la Dodoma, mradi wa kuimarisha miundombinu ya upimaji na ramani nchini, pamoja na mradi wa ujenzi wa daraja jipya la Salender, Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments