Na Ahmad Mmow, Lindi.
Wakati ununuzi wa korosho ghafi kwa msimu wa 2020/2021 ukielekea ukingoni, idadi ya wanunuzi wa korosho katika chama kikuu cha Lindi Mwambao imeendelea kuwa ndogo.
Katika mnada wa tisa kwa chama hicho kwa msimu wa 2020/2021 uliofanyika leo katika viwanja vya chama cha msingi cha ushirika cha Mnazimmoja ni kampuni moja pekee iliyoomba kununua Korosho ghafi kwenye chama hicho.
Chama hicho cha Lindi Mwambao, leo kilikuwa na jumla ya tani 683,071, wakati mnunuzi pekee ambae ni kampuni ya Hajari Trade Tanzania Ltd akiomba kununua tani 160 na kilo 482 pekee kwa bei ya shilingi 2,216 kila kilo moja katika ghala la Ilulu. Bei ambayo wakulima waliikubali.
Hali hiyo inafanana na mnada wa nane uliofanyika juma lililopita, ambao ulifanyika katika kijiji cha Mtua. Ambapo tani 472,415 kati ya tani 708,959 ndizo zilinunuliwa. Huku tani 236,544 zikikosa mnunuzi.
Kwenye mnada huo wa tisa ghala la Nangurukuru lina tani 48,358 za daraja la kwanza, na tani 44,753 za daraja la pili. Ghala Ilulu tani 160,482 za daraja la kwanza na tani 120,732 za daraja la pill. Wakati ghala la Bucco lina tani 45,966 za daraja la kwanza na tani 119,183 za daraja la pili. Ambapo ghala la Msajili wa Hazina lina tani 91,709 na daraja la pili tani 51,888.
Akizungumza baada ya wakulima kukubali kuuza kwa bei iliyoombwa na mnunuzi huyo, makamo mwenyekiti wa Lindi Mwambao, Rashid Masoud alitoa wito kwa bodi ya korosho (CBT) ambayo inadhamana ya kusimamia tasnia ya korosho nchini ijitahidi kutafuta soko ili Korosho zisizo nunuliwa ziweze kununuliwa.
Alisema chama hicho kipo tayari kushirikiana na bodi katika kuhakikisha changamoto ya soko inatatuliwa ili wakulima ambao wametumia raslimali zao kuzalisha zao hilo wananufaika na kazi waliyofanya.
Alibainisha kwamba hali hiyo inawakatisha tamaa wakulima nakusababisha mahudburio wa wakulima kwenye minada kuwa ndogo. Huku akiweka wazi kwamba wakulima wa wilaya ya Kilwa ambao korosho zao zipo katika ghala la Ilulu ni waathirika wakubwa wa hali hiyo. Kwani takribani minada minne hakujanunuliwa korosho kutoka katika ghala hilo.
Aidha Msoud alitoa wito kwa viongozi na watendaji wa vyama vya msingi( AMCOS) wasikubali kupokea Korosho zisizo na ubora. Jambo ambalo chama chake linasisisitiza mara kwa mara. Huku pia akiwataka waendesha maghala wasipokee korosho zisizo na ubora.
Kwa upande wake mwakilishi wa mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho katika mnada huo, Christopher Mwaya licha ya kusikitishwa na hali hiyo na kuahidi kushirikiana na chama kikuu kutatua changamoto hiyo alitoa wito kwa wakulima washiriki kikamilifu kwenye minada ili wafanye uamuzi sahihi wa kuuza au kutouza korosho zao.
Alisema kitendo cha wakulima kushindwa kushiriki kikamilifu minadani kinaweza kusababisha uamuzi wa kuuzwa korosho zao kufanywa na wanunuzi. Kitendo ambacho hakikubaliki.
0 Comments