Na Thabit Madai, Zanzibar.
KUKAMILIKA kwa Ujenzi wa kiwanda cha kusarifu mwani cha Chamanangwe mkoa wa Kaskazini Pemba, kunatarajiwa kulipandisha thamani zao hilo kwa kuinua hali za maisha ya wakulima pamoja na kuinua pato la Taifa.
Akifungua mafunzo ya wakufunzi wa wakulima wa mwani leo katika ukumbi wa Shirika la Biashara Zanzibar (ZSTC),Makonyo wilaya ya
Chake chake Mkoa wa Kusini Pemba, Waziri wa Kilimo,Umwagiliaji,Maliasili na Mifugo Zanzibar, Soud Nahoda Hassan amesema kiwanda hicho
kitakuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima wa mwani ambapo kwa miaka mingi wamekosa tija kutoka na bei ndogo wanaolipwa kutoka kwa kampuni zinazosafirisha zao hilo.
Waziri Nahoda aliekuwa akimwakilisha Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar alisema kwamba,Mwani unafaida nyingi kwa matumizi ya binadamu ambapo hutengenezea bidhaa mbalimbali zikiwemo Sabuni, Mafuta na manukato.
"Mahitaji ya Mwani yataongezeka kutokana na maamuzi ya Serikali ya ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kujenga kiwanda cha Kusarifu mwani cha
Chamanangwe ambapo itaongeza thamani ya zao hilo pamoja na kuenda sambamba na sera ya nchi kukuza uchumi wa kupitia bahari (Uchumi wa buluu)," Alisema Waziri Nahoda.
Alifahamisha kwamba,Kiwanda hicho kinachoendelea kujengwa kitakuwa na uwezo wa kusarifu tani 30,000 za mwani mkavu kwa mwaka kiwango ambacho
ni kikubwa hivyo hali hiyo itawalazimu wakulima waongeze jitihada katika uzalishaji kufikia kiwango hicho.
Waziri Nahoda aliongeza kuwa, hadi kufikia mwaka 2016 kiwango cha mwani kinacho sarifiwa visiwani Zanzibar kwa mwaka ni tani 16,000 hivyo wakulima watarajie manufaa makubwa ikiwemo kuongezeka kwa bei ya mwani.
Alisema,Serikali imechukua juhudi kubwa katika kukuza zao hilo kutokana na kutoa mchango mkubwa wa kukuza uchumi wa nchi na manedeleo endelevu kwa jamii.
Nae Mkurugenzi mkuu wa taasisi ya Utafiti wa Sera za maendeleo na umasikini (REPOA) Dk. Donald Mmari alisema lengo la taasisi yao ni kuunga mkono juhudi za Serikali
kwa kuwapatia utaalamu wakulima wa mwani utakao wezesha kupatikana mazao yenye thamani na tija.
"Zao la mwani lina nafasi kubwa ya kubadilisha maisha ya wakulima wa zao hilo endapo litashughulikiwa kitaalamu na kutumia vifaa vya kisasa," alisema Dk. Donald Mmari.
Alisema kupitia mafunzo hayo waliyoandaa watawawezesha wakulima kujua mbinu za kulima zao hilo katika maji ya kina kirefu ili kuepusha mwani kushambuliwa na wadudu na kupata kiwango kilicho bora.
Aidha alieleza mafunzo hayo yatasaidia Wakufunzi kwenda kufundisha wakulima namna bora ya kukuza na kuendeleza kilimo cha mwani na kupata soko la uhakika.
Nae Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda,Juma Reli alisema, Mafunzo hayo ya yatawawezesha wakulima kufahamu mbinu za kupanga mashamba yao katika kinakirefu cha mwanzo.
Aidha alisema mafunzo hayo yatawasaidia kuwafahamisha wakulima namna ya kuweza kuchagua mbegu bora za mwani pamoja na kuvuna zao la mwani ili liwe bora na lenye thamani kwa watumiaji.
Hata hivyo alisema Wizara ya biashara kupitia kamati zake za maendeleo inafanya kazi kubwa kuhakikisha kuwa zao la mwani linakuwa na kuwanufaisha wananchi kwa kuongeza fursa mbalimbali za ajira.
"Kamati hii inafanya kazi kubwa ili kuongeza thamani na tija zao la mwani ambapo tumeanza na kuandaa mafunzo haya ambapo awali yamefanyika hapa Pemba na yanatarajiwa kufanyika na kisiwani
Unguja," alieleza Katibu Mkuu Juma Reli.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa Mafunzo hayo,Fatma Muhammad Makame alipongeza jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar pamoja na taasisi wa taasisi ya Utafiti wa
Sera za maendeleo na umasikini (REPOA) kwa kuwaandalia mafunzo yenye lengo kuwainua wakulima wa zao hilo visiwani humo.
Mafunzo hayo yanayowashirikisha wakufunzi wa wakulima wa mwani 30 ambayo yamepangwa kufanyika siku 9 ambapo itahusisha nadharia na vitendo
0 Comments