F Waziri Mifugo na Uvuvi aanza kazi rasmi, ahamasisha ufugaji wa samaki kwenye mabwawa | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Waziri Mifugo na Uvuvi aanza kazi rasmi, ahamasisha ufugaji wa samaki kwenye mabwawa



Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema ufugaji wa Samaki katika Mabwawa na Vizimba ukihamasishwa na kupewa msukumo mkubwa utasaidia kuongeza wingi wa samaki na utasaidia kupunguza uvuvi harama katika maji ya asili.

Ndaki aliyasema hayo alipotembelea Shamba la Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda lilipo jijini Dodoma Disemba 9, 2020.

Alisema kuwa serikali imefanya kazi kubwa katika kuimarisha sekta ya uvuvi ikiwemo ufugaji wa samaki katika vizimba na mabwawa lakini alisisitiza kuwa kunahitajika kuongeza nguvu na jitihada zaidi kuwahamasisha wananchi kujiingiza katika ufugaji wa samaki ili kujiongezea kipato na kupunguza utegemezi wa mazao ya samaki kutoka katika maji ya asili.

“Ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba na mabwawa utatusaidia kupunguza purukushani kati ya serikali na wavuvi haramu kwa sababu kama samaki wengi watapatikana kupitia ufugaji, watu hawataona haja ya kuhangaika na uvuvi usio na tija,” alisema Ndaki huku akiongeza kuwa;

“Tunahitaji kufanya jitihada zaidi kutangaza na kuhamasisha ufugaji wa samaki hasa kwa kutumia mabwawa ya gharama nafuu kama malambo ili wafugaji na wananchi kwa ujumla waweze kuona ufugaji huo ni nafuu na wanaweza kupata kipato kupitia kazi hiyo,” alisema Ndaki

Aliongeza kwa kusema kuwa hamasa ya ufugaji wa samaki ikiwa kubwa na wanunuzi nao wataongezeka jambo ambalo litapelekea pia kuongezeka kwa wawekezaji katika vyakula na ukuzaji wa vifaranga na hivyo kutatua changamoto iliyopo sasa ya uchache wa vifaranga na vyakula vya samaki.

“Ndani ya Wizara tutaona namna ya kujipanga ili tuendelee kuiwezesha zaidi hii sekta ya uvuvi iweze kukua zaidi na kuongeza kipato cha watu wetu na kutoa mchango mkubwa katika pato la Taifa,” alisisitiza Ndaki

Awali wakati akimkaribisha Waziri huyo Mteule Shambani hapo, Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda alisema kuwa changamoto kubwa anayoipata shambani hapo ni kutopatikana kwa urahisi kwa vifaranga vya samaki pamoja na chakula cha uhakika.

“Hapa tunapata changamoto ya vifaranga vya samaki havipatikani kwa urahisi lakini pia hakuna mahala ambapo unaweza kusema hapa wanazalisha chakula cha uhakika,” alisema Pinda

Aliongeza kwa kusema kuwa pamoja na jitihada kubwa za serikali katika kuimarisha sekta ya uvuvi lakini angetamani kuona sekta hiyo inaendelea kupewa nafasi kubwa zaidi hasa katika ufugaji wa samaki wa kutumia mabwawa na vizimba kwani utasaidia wananchi kujipatia kipato na kukuza uchumi wao. 

Naye, Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah alisema kuwa kwa sasa serikali inaendelea kukarabati vituo vya uzalishaji wa vifaranga ili kuongeza uwezo wa kuzalisha ikiwemo kuimarisha mashamba darasa ili kufundisha watu namna ya kutengeneza chakula cha samaki na ufugaji wa samaki.

Dkt. Tamatamah aliongeza kuwa serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika uzalishaji wa vifaranga na uzalishaji wa Chakula na kwa sasa wapo katika mazungumzo na serikali ya Misri ili Kampuni zao ziweze kuwekeza katika uzalishaji mkubwa wa vifaranga na vyakula vya samaki hapa nchini.

Ndaki alifanya ziara hiyo muda mfupi baada ya kuapishwa rasmi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Disemba 9, 2020, na kazi yake ya kwanza ilikuwa kutembelea machinjio ya Dodoma na Shamba la Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda.

Post a Comment

0 Comments