VICTOR MASANGU, PWANI
Afisa elimu wa Mkoa wa Pwani Hadija Mcheka amewataka wakuu wote wa shule za msingi na sekondari kuhakikisha wanaweka vizuri miundombinu ya mazingira ya shule zao kuwa safi na salama ikiwemo uwepo wa vitakasa mikono ambavyo vitaweza kuwasaidia wanafunzi kunawa ili kuondokana na magonjwa ya mlipuko.
Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini Kwake kuhusiana na maandalizi ya kuelekea katika kufungua shule Afisa elimu huyo alibainisha kwamba walimu wote kwa sasa wanatakiwa kuweka mikakati ambayo itaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa wanafunzi pindi wanapofungua shule zao waweze kusoma katika mazingira masafi.
“Kipindi cha likizo kwa sasa ndio kimemalizika kwa wanafunzi wetu wa shule mbali mbali za msingi na sekondari katika Mkoa wetu wa Pwani kwa hivyo mimi napenda kutumia fursa hii kwa ajili ya kuweza kuwakumbusha walimu wakuu wote wa shule husika kuweka mazingira ya ufasi katika maeneo yote ya shule ikiwemo kuwa na vitakasa mikono ili wanafunzi waweze kuepukana na magonjwa mbali mbali ya mlipuko,”alisema Hadija.
Pia aliongeza kuwa serikali ya awamu ya tano lengo lake kubwa ni kihakikisha kwamba wanafunzi wanasoma katika mazingira ambayo ni salama na rafiki hivyo kunahitajika kufanyike usafi wa mara kwa mara katika maeneo mbali mbali ikiwemo kufyaka nyasi, kusafisha madarasa pamoja na kusafisha katika maeneo ya vyooni.
“Shule zetu zilikuwa zimefungwa lakini zinafunguliwa siku ya jumatatu, kwa hivyo natambua baadhi ya maeneo kutakuwa na uchafu hivyo ninawahimiza tena wakuu wote wa shule kulitilia mkazo suala hili kwani likifumbiwa macho linaweza kusababisha kutokea kwa mlipiko wa magonjwa mabi mbali ikiwemo kuumwa na matumbo pamoja ana kipindpindu,”alisema.
Kadhalika Afisa elimu huyo alisisitiza kuhusiana na usafi wa vyoo vya shule pamoja na vyoo vya walimu viwe katika hali ya usafi, na kwamba kwa kufanya hivyo kutaweza kusaidia kwa kiasi kukubwa kupunguza au kuamaliza kabisa changamoto ya magonjwa ya milipuko kwa wanafunzi pamoja na walimu na kuweza kusoma katika hali nzuri.
Katika hatua nyingine aliongeza kuwa kuwepo kwa milipuko ya magonjwa mbali mbali kunatokana uchafu hivyo pia amewataka hata wamiliki wa shule binasfi kuliangalia hilo kwa jicho la tatu katika kufanya usafi wa mazingira katika maeneo yote yanayozunguka shule pamoja na ndani ya madarasa ambayo wanasomea wanafunzi.
Pia alifafua kwamba changamoto nyingine ambayo inaweza kusababisha watoto kutokwenda shule ni kwa ajili ya kupata magonjwa mbali mbali ya milipuko hivyo ana imani kwamba mazingira ya mashuleni yakiwa masafi kwa asilimia kubwa pia kutasaidia katika kuwafanya wanafunzi waweze kusoma vizuri na kuongeza kiwango cha ufaulu.
0 Comments