Chama kikuu cha upinzani katika Jamhuri ya Congo kimesema kitasusia uchaguzi uliopangwa kufanyika Machi 21. Kwenye uchaguzi huo Rais Denis Sassou Nguesso aliyepo madarakani kwa miongo kadhaa anawania kuchaguliwa tena.
Nguesso mwenye umri wa miaka 77 ameshikilia madaraka kwa miaka 36 sasa na hivyo kuwa mmoja wa viongozi waliodumu kwa muda mrefu madarakani ulimwenguni. Katibu wa kwanza wa chama cha upinzani cha Pan-African Union for Social Democracy (UPADS) Pascal Tsaty Mabiala amesema kufanyika kwa uchaguzi huo wa urais isiwe sababu ya kuligawanya taifa kama ilivyokuwa zamani na hivyo chama chake kimeamua kutoshiriki katika uchaguzi huo.
Chama hicho cha UPADS cha aliyekuwa rais wa zamani Pascal Lissouba ndicho pekee cha upinzani chenye uwakilishi bungeni. Congo Brazaville imo kwenye mgogoro mkubwa wa kiuchumi uliosababishwa na kushuka kwa bei ya mafuta, deni la muda mrefu pamoja na athari za janga la corona.
0 Comments