Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alisema Watanzania hawanabudi kuongeza bidii na Mikakati ya muda mfupi na mrefu katika kuona Lugha ya Kiswahili inaendelea kuwa kimbilio la watumiaji Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.
Alisema hadhi iliyofikia Lugha hiyo hivi sasa imefungua Milango kwa Wataalamu wa Kiswahili kufaidika kutokana na fursa zinazopatikana kwenye maeneo ya Ukalimani, Tafsiri, Uandishi wa Vitabu, Uhariri na ufundishaji wa Kiswahili kwa Wageni.
Akiyafunga Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Mwaka huu katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma Mheshimiwa Hemed Suleiman alisema Kiswahili ni bidhaa inayouzika Sokoni na tayari imeanza kutumika katika Taasisi za Kimataifa ikiwemo ile ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kiuchumi ya Mataifa ya Kusini mwa Bara la Afrika {Sadc}.
Alisema Watanzania wenye uwezo wana fursa ya kushirikishwa wakati huu kwa kuanza kufungua vituo vya kufundishia Lugha ya Kiswahili na Utamaduni katika Mataifa yenye Afisi za Kibalozi za Tanzania ikiangalia zaidi kwa kuanzia na Mataifa ya Sadc.
“ Kiswahili ni Miongoni mwa Tunu za Taifa letu na kimesaidia kutuunganisha na kutuwezesha kuwa wamoja na kudumisha Mshikamano wa Taifa. Hivyo basi ni wajibu wetu kukiendeleza mahali popote tulipo”. Alisema Mheshimiwa Hemed Suleiman.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha zaidi Uchumi wa Taifa unaokwenda sambamba na uuzaji wa bidhaa ya Kiswahili ambayo Mataifa mengine hushawishika kuipenda kutokana na Kasi ya ukuwaji wa Uchumi huo.
Alisema upo ushahidi wa wazi wa Mataifa mengi Duniani ikiwemo Tanzania na Zanzibar kwa Ujumla yamekufungua Vituo vya kujifundishia Lugha ya Kichina kutokana na Mataifa hayo kuwa na haja ya kufanya Biashara na China iliyokua Kiuchumi hivi sasa.
Mheshimiwa Hemed Suleiman alieleza kwamba Serikali zote Tanzania zinazingatia kutilia mkazo suala la kukiendeleza Kiswahili kwa kuzibaini na kuzitumia fursa mbali mbali za Kiswahili zinazopatikana kutoka katika Mataifa yenye Watu wanaohitaji kujifunza Lugha hiyo adhimu.
Kwa kuzingatia hayo alisema Serikali hizo zitaendelea kubeba jukumu la kushirikiana na Baraza la Kiswahili la Taifa Tanzania { BAKITA} na Baraza la Kiswahili Zanzibar {BAKIZA}, Wadau,Taasisi na Idara za Kiswahili katika kuhakikisha Watanzania wenye weledi wa Kiswahili wanafaidika na Lugha hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amempongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kwa kutunukiwa Nishani ya Juu ya Shaaban Robert kutokana na mchango wake mkubwa katika kukiendeleza Kiswahili tokea alipoingia madarakani mnamo Mwaka 2015.
Aidha Mheshimiwa Hemed alizishukuru na kuzipongeza Taasisi na Watu mbali mbali waliobahatika kupata Tuzo na kutambuliwa kwa mchango wao mkubwa wa kuisimamia Lugha hiyo na ni vyema ikawa kichocheo kwa Waswahili wengine kuiga mfano wao.
Mapema akitoa Taaifa ya uwamuzi wa Baraza la Kiswahili Tanzania kumtunuku Tuzo ya Shaaban Robert Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kutokana na msimamo wake wa Kukiendeleza Kiswahili Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza hilo Dr. Method Samuel alisema vigezo maalum vimewekwa ili kumbaini Mtu anayestahiki kupata Nishati hiyo.
Dr. Method Samuel alisema vigezo hivyo ni pamoja na muhusika kuandika Vitabu Vingi, kuvichapisha, kusaidia kuleta mabadiliko ya maendeleo ya Lugha, Uongozi bora na kukiendeleza Kiswahili mambo ambayo Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.Magufuli amefikia sifa hizo.
Alisema Rakba yake kubwa Dr, Johm Pombe Magufuli katika Utashi wa Kisiasa kwenye harakati zake za kukieneza Kiswahili ulikuwa mkubwa ulioambatana na juhudi za Taasisi husika zilizozaa matunda ya upatikanaji wa Kanuni za Uendeshaji wa Baraza la Kiswahili Tanzania {BAKITA}.
Dr. Samuel alifafanua kwamba ziara ya mwanzo ya Rais wa Jamuhuri yaMuungano wa Tanzania katika Nchi za Kusini mwa Bara la Afrika mara baada ya kuchaguliwa Rais wa Tanzania alijitahidi kukinadi Kiswahi kitendo ambacho kimeleta mafanikio makubwa.
Alibainisha kwamba mafanikio hayo yalionekana wakati wa Mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kiuchumi ya Mataifa ya Kusini mwa Bara la Afrika yaliyofanyika Jijini Dar es salaam alipoteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo ambapo alitumia Lugha ya Kiswahili akiwa na azma ile ile ya kuikuza Lugha hiyo.
Mwenyekiti huyo wa Baraza la Kiswahili la Taifa {BAKIZA} alielezea faraja ya Washirika wa Kiswahili Tanzania kutokana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 – 2025 Ibara ya 235,236,237 na 238 iliyoweka msisitizo wa kuendelezwa Lugha ya Kiswahili.
Akimkaribisha Mgeni rasmi kuyafunga Maadhimisho hayo ya Siku ya Kiswahili Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Abdalla Ulega alisema Watanzania Wana kila sababu ya kumshukuru Rais John Pombe Magufuli kwa kuwa kinara wa kusimamia ukuaji wa Lugha ya Kiswahili.
Mh. Ulega alisema pongezi hizo kwa vile zina umuhimu mkubwa na itapendeza kama historia hiyo itabakia katika kumbukumbu itakayotumika kwa vizazi vya sasa na vile vijavyo.
Katika hafla hiyo ya ufungaji wa Maadhimisho hayo ya Siku ya Kiswahili Tuzo na Vyeti mbali mbali vilitolewa kwa Washirika wa Lugha ya Kiswahili vikiwemo vyombo vya Habari vya Redio, Tv na Magazeti.
Wengine ni Wanafunzi wa Skuli za Sekondari, vyuo Vikuu, wahadhiri wa Vyuo vya Elimu ya juu pamoja na Taasisi zilizosaidia kufanikisha Maadhimisho hayo ambazo ni pamoja na TMA, Baraza la Mazingira, PSSF, TCRA, NHC, TRA, TBC, DAWASA, Long Publisher, Mamlaka ya Usafirishaji wa Ardhini pamoja na Chuo Kikuu Shirikishi Dar es salaam.
Ujumbe wa Mwaka huu wa Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili unaeleza “ Bidhaisha Kiswahili kwa Maendeleo Endelevu ya Tanzania” . Ujumbe huu umezingatia ukweli usiopingika kwamba Kiswahili hivi sasa ni Bidhaa inayouzika sokoni na kutumika kwa Maendeleo ya Taifa.
0 Comments