Safari ya maisha ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, imefikia mwisho jioni ya leo, mara baada ya mwili wake kupumzishwa katika nyumba yake ya milele kijijini kwake Mtambwe, visiwani Pemba.
Mapema leo asubuhi mwili wa Maalim Seif, uliswaliwa katika msikiti wa Maamur Upanga jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, na kisha baadaye ulisafirishwa hadi Zanzibar na kupelekwa katika viwanja vya Mnazi Mmoja kwa ajili ya Dua maalum.
Mazishi ya Maalim Seif, yameongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi, pamoja na viongozi wengine mbalimbali wa serikali na wa vyama kutoka vyama mbalimbali vya kisiasa nchini.
Maalim Seif alifariki dunia Februari 17, 2021, katika hospitali ya Taifa Muhimbili alipokuwa anapatiwa matibabu.
0 Comments