Rais Xi Jinping asema China imefikia miujiza ya kibinaadamu kuondowa umasikini uliotitia


Rais Xi Jinping wa China ametangaza kwamba nchi yake imefanikiwa kile alichokiita kuwa ni 'miujiza ya kibinaadamu' kwa kutokomeza umasikini uliotitia kwenye maeneo ya vijijini. 

Katika sherehe iliyofanyika mjini Beijing hivi leo, Xi aliwatunukia medali maafisa kutoka jamii za vijijini, wengine wakiwa wamevalia mavazi ya kimila, huku akiahidi kuchangiana kile alichokiita "kigezo cha China" na mataifa mengine yanayoendelea.

Xi amewaambia maafisa hao kwamba hakuna taifa ambalo limeweza kuwainuwa mamilioni ya watu kutoka kwenye umasikini ndani ya kipindi kifupi kama ambavyo China imefanikiwa kufanya. 

Mwaka jana, China ilidai kwamba imefanikiwa kutimiza lengo lake la muda mrefu la kuwafanya raia wake wote kuondoka kwenye mstari wa chini wa umasikini wa mapato ya dola 2 na senti 30 kwa siku. 

Benki ya Dunia inasema China imefanikiwa kuwainuwa zaidi ya watu milioni 800 kutoka umasikini uliotitia tangu ilipogeukia mageuzi ya soko kwenye miaka ya 1970.

Post a Comment

0 Comments