F Taha yaja na mwarobaini ajira kwa vijana Mwanza | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Taha yaja na mwarobaini ajira kwa vijana Mwanza

 


Wakati vijana wakilalamikia uhaba wa ajira nchini, taasisi inayojishughulisha na uzalishaji matunda na mboga mkoa wa Mwanza (Taha) imeanzisha shamba darasa kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 litakalowapatia mafunzo na ujuzi wa namna ya kuzalisha na kusindika matunda na mboga.


Akizungumza Machi 16, 2021 katika shamba darasa lililoko Malimbe Kata ya Luchelele mkoani hapa ofisa kilimo kutoka Taha, Raymond Gervas amesema endapo vijana wakiwemo wasomi wa elimu ya juu watajitokeza kupewa elimu ya kilimo na usindikaji wa mazao hayo huenda wakatatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana.


“Hapa kwenye shamba darasa tuna vijana 10 ambao wamelima zao la nyanya nusu hekari na wanategemea kuvuna tenga zaidi ya 200 za nyanya ambazo kwa bei ya sokoni kwa sasa kila tenga inauzwa Sh20, 000 kwa hiyo kama wakisimamiwa vyema vijana hawa watapata na mtaji wa kuanzisha biashara nyingine,” amesema Gervas.


Gervas amesema taasisi hiyo inatoa mafunzo ya uzalishaji wa mazao hayo kwa kushirikiana na Shirika la Plan International chini ya mradi wa vijana, Maisha na Kazi ambapo vijana wanapewa mafunzo na vifaa vya kuwasaidia kuzalisha mazao hayo.


Meneja wa Mradi huo kutoka Shirika la Plan International, Nelson Msikula amesema mradi huo wa miaka minne ulianza mwaka 2018 na unategemewa kukamilika Desemba 2022 ambapo wanalenga kutoa mafunzo hayo kwa vijana 1,000 kutoka wilaya ya Nyamagana na Ilemela jijini Mwanza.


“Tunategemea asilimia 55 ya wanufaika wa mafunzo haya wawe wanawake, asilimia tano wawe watu wenye ulemavu na asilimia zinazosalia watakuwa vijana wa kiume wakiwemo wanaotoka katika kaya maskini na wasomi wasiyo na ajira,” amesema Msikula.


Naye Mustahiki Meya wa Jiji la Mwanza Costantine Sima amewaomba vijana wanaotoka katika kaya maskini kujitokeza kupata mafunzo hayo huku akitoa wito kwa vijana wenye ujuzi huo kuutoa kwa vijana wengine ili kuongeza mnyororo wa ujuzi na kupunguza tatizo la ajira nchini.

Post a Comment

0 Comments