Na John Walter-Manyara
Viongozi wa dini, serikali , Wananchi na chama cha Mapinduzi mkoa wa Manyara kuungana leo machi 24,2021 kufanya ibada ya kumuombea Hayati John Pombe Magufuli, Rais Samia Hassan na Taifa.
Ibada hiyo inatarajiwa kuanza saa nne kamili asubuhi katika eneo la wazi la stendi ya zamani mjini Babati.
Akizungumzia ibada hiyo Katibu Mwenezi wa chama cha Mapinduzi mkoa wa Manyara Jacob Siay amesema wameamua kufanya hivyo kwa kuwa wengi hawakupata nafasi ya kuuaga mwili wa mpendwa wao Hayati Dr. Magufuli.
Siay amesema Chama cha Mapinduzi baada ya kupokea taarifa za msiba, walitengeneza utaratibu wa kuvaa sare za chama na kuvaa kitambaa cheusi mkono wa kushoto na kuwa na kitabu cha kumbukumbu katika ofisi zote za chama.
"Tumeamua kuandaa ibada ya pamoja ili kushiriki katika kumuombea kwa Mungu apumzike salama, lakini pia kumuombea rais Samia Suluhu Hassan na taifa kwa ujumla" alisema Siay
Amesema jambo hilo wanalolifanya sio la chama tu bali ni la wananchi wote hivyo amewaomba kujitokeza kwa wingi katika ibada hiyo maalum ya kumuombea Hayati Dr.John Pombe Magufuli apumzike kwa amani.
"Hapa Manyara Magufuli amefanya mambo mengi, ametujengea barabara za lami, miradi mikubwa ya maji, huduma za afya na mengine mengi," amesema Siay.
Amesema Watanzania wanapaswa kumuenzi Magufuli kwa mambo mengi mema aliyofanya kwa Watanzania.
0 Comments