Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu mfanyabiashara, Yericko Nyerere kulipa faini ya Sh5 milioni au kwenda jela miaka mitatu baada ya kukutwa na hatia ya kuchapisha maneno ya uchochezi katika mtandao wa kijamii wa Facebook yenye lengo la uvunjifu wa amani.
Hukumu hiyo imetolewa leo Jumanne Machi 23, 2021 na hakimu mkazi mkuu wa mahakama hiyo, Kassian Matembele wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya kutolewa hukumu.
Akisoma hukumu hiyo, Matembele amesema ameridhishwa na ushahidi wa mashahidi saba wa upande wa mashtaka pamoja na vielelezo vinne vilivyotolewa mahakamani hapo wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo.
"Mahakama hii imemtia hatiani mshtakiwa kama alivyoshtakiwa, Yericko unatakiwa kulipa faini ya Sh5 milioni au kwenda jela miaka mitatu na haki ya kukata rufaa iko wazi " amesema Matembele.
Awali, wakili wa Serikali, Ashura Mzava ameiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa kutokana na kitendo alichokifanya kuwa ni kinyume cha sheria na kinahatarisha amani kwa wananchi.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, mahakama ilitoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea kwa nini asihukumiwe adhabu hiyo.
Mshtakiwa huyo kupitia wakili wake, Hekima Mwasipu ameiomba mahakama hiyo impunguzie adhabu kwa sababu ana familia inayomtegemea.
Hata hivyo, Matembele alitupilia mbali maombi hayo ya upande wa utetezi na kumhukumu Nyerere kulipa faini na kama atashindwa atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela
Katika kesi ya msingi, Nyerere anakabiliwa na kesi ya jinai namba 188/ 2017.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Mei 28, 2017 katika jiji la Dar es Salaam.
Inadaiwa siku ya tukio kupitia akaunti yake ya kijamii ya Facebook aliandika maneno ya uchochezi, " Maazimio ya Baraza Kuu yalikuwa 1.Katiba Mpya 2.Tume huru 3.Bunge 4.Haki ya Kikatiba ya kuishi (Ben saanane) 5.Haki ya kikatiba ya kukutana na kuzungumza (mikutano ya hadhara ya kisiasa). Hayo ndio yatahubiriwa katika operesheni Ukuta. Baraza Kuu limeridhia kwa kauli moja kwamba vita rasmi ya kulikomboa taifa imezinduliwa na kama wewe Mtanzania unaogopa kulitetea Taifa hili kaa kando, nenda huko CCM ambako michemsho na supu vipo kwa wingi .....kula kwetu ni ukombozi wa Tanzania .......yaani sasa tunarejesha siasa za jino kwa jino uso kwa uso mguu kwa mguu, weka mguuni weka ugoko .....Ni mwisho kuishi kinyonge ni mwisho kulalamika ni mwisho watu wetu kutekwa au kuuawa, ni mwisho watu wetu kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara.....Tunasema sasa ni single touch double Manifestatio.”
Ilidaiwa kuwa maneno hayo, yanaweza kuleta uvunjivu wa amani na ni kinyume cha sheria.
0 Comments