F Bei mafuta ya kula yaongeza makali kwa wananchi | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Bei mafuta ya kula yaongeza makali kwa wananchi

 


Ongezeko la bei ya mafuta ya kula limezidi kuwa kilio kwa wananchi, hasa wenye kipato cha kawaida na wale wa chini, huku Serikali ikisema kuwa italitolea ufafanuzi suala hilo Jumanne ijayo.


Kupaa kwa bei ya mafuta kumekuwa kukiongeza bajeti ya ununuzi ya vyakula vya familia, huku mama lishe wakilalamika zaidi kutokana na ongezeko la gharama za uzalishaji wa vyakula vyao.


Mathalani dumu la lita tano la mafuta kwa sasa linauzwa Sh39,000 kutoka Sh18,000 iliyokuwa ikitumika takribani miezi minne iliyopita.


Mjini Moshi bei ya mafuta ya kula imezidi kupaa kutoka Sh5,000 kwa lita hadi kufikia Sh6,000 kwa lita moja.


Muuzaji wa duka la vyakula katika mji wa Moshi, Irene Mushi alisema mafuta walikuwa wanauza lita moja Sh4,700, lakini kwa sasa wanalazimika kuuza Sh5,500 hadi Sh6,000 kwa lita kutokana na bidhaa hiyo kupatikana kwa bei ya juu.


Alisema ndoo ya lita kumi wanauziwa Sh45,000 kwenye maduka ya jumla, suala linalosababisha hadi kumfikia mlaji iuzwe kwa bei ya Sh55,000.


ADVERTISEMENT

Jijini Mwanza, lita tano za mafuta ya kula zinauzwa kwa Sh28,000, lita 10 ni Sh43,500 na lita 20 zikiuzwa kwa Sh81,000.


Katika maduka ya mitaani lita moja ya mafuta inauzwa Sh1,800, nusu lita inauzwa Sh900, huku kibaba kimoja kikipimwa kwa Sh200.


Wilaya ya Bukombe mkoani Geita lita 20 za mafuta ya kula zinauzwa kwa Sh83,000, lita 10 zikiuzwa Sh45,000, bei ambazo ni za juu ikilinganishwa na bei za zamani.


Jijini Dodoma, bei imeendelea kubaki kama ilivyokuwa miezi mitatu kabla ambapo lita moja inauzwa kati ya Sh4,000 hadi 5,000.


Mmoja wa wauzaji wa mafuta hayo, Joyce Yohana alisema kuwa bei zinatofautiana kulingana na aina ya mafuta, kwani yapo anayouza kwa Sh4,500 na mengine anauza Sh5,000.


Muuzaji mwingine wa rejareja, Reuben Geofrey alisema lita moja ya mafuta hayo anauza kwa Sh4,000, na kuwa wateja watarajie bei kushuka, kwani wakulima wanakaribia kuvuna alizeti.


Kufuatia malalamiko hayo, Katibu Mkuu wizara ya viwanda na biashara, Profesa Riziki Shemdoe alisema kwa sasa mafuta yapo na suala la bei linafuatiliwa na kuahidi kutolea ufafanuzi wa kina suala hilo Jumanne, Aprili 6.


Jamila Shaibu, mkazi wa Buguruni jijini Dar es Salaam alisema kwa takribani wiki mbili sasa, baadhi ya vyakula amekuwa akivipika pasipo kuongeza mafuta kutokana na gharama ya bidhaa hiyo.


“Ninaweka mafuta kwenye mboga, ubwabwa siweki na wakati mwingine ninaweza kupika chakula bila mafuta. Wanangu wamezoea maana kama bajeti ya siku ni Sh3,000 huwezi kusema ununue mafuta pia, maana inabana,” alisema Jamila.


Hata hivyo, baadhi wananchi wameilalamikia Serikali, ambayo awali ilidai kuwa bei zingeshuka kufuatia meli zilizokuwa zikishusha mafuta bandarini. Mwanzoni mwa mwaka meli kadhaa zilishusha mafuta katika bandari ya Dar es Salaam, lakini imeelezwa kuwa bei bado imekuwa si rafiki kwa watumiaji.


Kwa mujibu wa aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe kwa mwaka mahitaji halisi ya mafuta ya kupikia nchini ni tani za ujazo 570,000 na kiasi kinachozalishwa nchini ni tani 205,000, hivyo kuna upungufu wa tani 365,000 ambazo huagizwa kutoka nje ya nchi.


Post a Comment

0 Comments