WIZARA ya Maliasili na Utalii imetoa muda wa siku saba kwa uongozi wa mkoa wa Killimanjaro kuhakikisha unarekebisha kasoro zilizo kwenye mikataba ya shamba la kutunzia wanyamapori yatima la Makoa kabla ya kupewa kibali cha kuleta Simba kutoka nje ya nchi kwa ajili ya matunzo.
Akizungunza mara baada ya kutembelea shamba la Wanyamapori la Makoa , Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro amesema kuwa shamba hilo linapokea wanyamapori yatima na majeruhi kutoka kwenye hifadhi zote hapa nchini.
Amesema kutokana na umuhimu wa shamba hilo, ipo haja ya Serikali ya Mkoa kusaidia Chama cha Ushirika cha Urudu Makoa ili kiweze kufahamu namna sahihi ya kuingia mikataba yenye tija kwa Taifa.
“Nimetoa siku saba kwa viongozi wa Mkoa kuhakikisha wanakisaidia Chama cha Ushirika cha Uduru Makoa ili waweze kurekebisha kasoro zilizojitokeza kwenye mikataba ya uwekezaji pia wafahamu, ukomo wa mikataba na nani wanaingia nae mikataba hiyo na manufaa yake kwa vyama vya ushirika na Taifa kwa ujumla,” Amesisitiza Dkt. Ndumbaro.
Aidha, amesema ziara yake imelenga kutazama bustani hiyo inayotunza wanyamapori waliojeruhiwa au yatima ambao hutunzwa hadi na baadaye kurudishwa kwenye hifadhi pindi wanapokuwa au kurejea katika hali zao za kawaida.
Dkt. Ndumbaro amesema kuwa Wizara imejiridhisha pasipo shaka malezi na mazingira ya utunzaji wa wanyamapori hao yanaridhisha licha yakuwa bado kuna ukakasi katika mikataba waliyoingia.
” Mkataba walioingia kati ya Makoa na Mwekezaji huyo haijafuata misingi ya kisheria na leseni iliyotolewa imetolewa kwa mtu binafsi ambaye si muhusika wa shamba hilo, hivyo tumewaagiza Mkoa kukamilisha kasoro hizo mara moja, wakikamilisha taratibu zote walete maombi yao yakuleta wanyamapori kutoka nje ya nchi tutayashughulikia, “amesema Dkt. Ndumbaro.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Anna Mghwira amesema kumekuwa na ukakasi wa kufahamu Mwekezaji halisi ni nani ili kuingia mkataba jambo ambalo baada ya Waziri kufika kila kitu kimekuwa wazi.
” Muda wa siku saba tuliopewa unajitosheleza maana kila kitu kipo ni kiasi cha kujipanga kulingana na Sheria na taratibu kwa mwongozo wa wataalamu wetu,” amesema
Naye mbunge wa jimbo hilo Mhe. Saashisha Mafuwe amesema ujio wa Waziri Ndumbaro umesaidia kufungua ukurasa mpya wa utendaji wa vyama vya ushirika vianze kuingia mikataba itakayoleta mabadiliko na faida kwa Taifa.
“Ombi langu kwa Mawaziri wengine kufika jimboni hapa kwani upo umuhimu mkubwa wa Serikali kutupia jicho la pekee hasa katika mikataba ya vyama vya ushirika,” amesema Mhe. Saashisha
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika Uduru Makoa,Saeli Mafuwe amesema wamepokea maelekezo na maagizo ya wizara husika na watayafanyia kazi kwa mujibu wa taratibu, kanuni na sheria.
” Mkataba wetu unakataza Mwekezaji kumpangisha Mwekezaji mwingine, na hapa ndicho kilichotokea, tutakaa na timu ya wataalamu kutoka wilayani na mkoani, ili kuona namna ya kutatua matatizo haya,”
Katika ziara hiyo walikuwepo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja, Katibu Mkuu, Dkt. Allan Kijazi na Wataalamu mbali mbali kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ambazo ni TAWIRI, TAWA na TANAPA.
0 Comments