Kamati maalumu ya tathmini ya ugonjwa wa corona (Covid-19) nchini imekamilisha kazi yake na kukabidhi ripoti kwa Rais Samia Suluhu Hassan leo Mei 17 ikiwa na jumla ya mapendekezo 19.
Rais Samia alitangaza kuunda kamati hiyo Aprili 6 ikiwa ni wiki chache baada ya kuapishwa, huku msisitizo mkubwa ukiwa katika kupambana na ugonjwa huo kwa njia za kisayansi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 17 Ikulu jijini Dar es Salaam, mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Said Aboud kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) alibainisha mapendekezo waliyoyatoa kwa Serikali.
Miongoni mwa mapendekezo hayo ni Serikali kuhuisha mipango ya dharura katika kukabiliana na majanga, Serikali kutoa taarifa za uwepo wa ugonjwa wa corona nchini na wataalamu wa afya watimize wajibu wao kitaalamu kwa kuzingatia weledi, miiko na maadili.
Amesema Tanzania ishiriki katika kufanya maamuzi na itekeleze maazimio ya kikanda na kimataifa, Serikali iendelee na hatua kuelekea kuruhusu matumizi huru ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa corona.
“Pamoja na mapendekezo hayo, kamati huru ya kitaifa ya chanjo na mamlaka ya dawa na vifaa tiba (TMDA) ziendelee kushirikishwa katika kutoa ushauri na kudhibiti chanjo hizo.
“Kipaumbele cha utoaji wa chanjo dhidi ya Covid-19 nchini kiwe katika makundi ya wahudumu wa vituo vya kutolea huduma za afya na watumishi walio katika mstari wa mbele mathalani watumishi wa sekta ya utalii, hoteli, mipakani, viongozi wa dini na mahujaji,” amesema Profesa Aboud.
Amebainisha makundi mengine kuwa ni pamoja na wazee kuanzia miaka 50, watu wazima wenye maradhi sugu, watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama na wasafiri wanaokwenda nje ya nchi, Serikali ianze mchakato wa kupata chanjo.
Mapendekezo mengine ya kamati ni Serikali kujenga uwezo wa ndani wa utambuzi wa maambukizi ya virusi vya corona, itoe takwimu sahihi za ugonjwa wa covid-19 nchini kwa umma na Shirika la Afya duniani (WHO) na Wizara ya Afya ikamilishe mwongozo mpya wa matibabu ya corona.
Amesema wanapendekeza matumizi ya tiba mbadala na tiba asili yazingatie misingi ya kisayansi, Serikali itoe fursa kwa wanasayansi kuendelea kufanya tafiti kwa mufuata miiko na maadili na Serikali iendelee kuzingatia mazingira ya kitanzania katika udhibiti wa ugonjwa wa Covid-19 katika kuweka au kutokuweka lockdown.
Vilevile, wamependekeza Wizara ya Fedha na Uchumi ifanye tathmini ya athari za kiuchumi zilizosababishwa na Covid-19; Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ziendelee kushirikiana katika kukabiliana na corona.
Idara ya maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu pia iendelee kutekeleza jukumu la uratibu na kutoa rasilimali husika katika majanga ya kitaifa na kimataifa, Serikali ikamilishe malipo ya madeni ya watoa huduma na watumishi waliokuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na Covid-19 na Serikali iendelee kushirikisha wadau mbalimbali.
“Serikali iendelee kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, wadau wa maendeleo, sekta binafsi na vyombo vya habari katika mapambano dhidi ya janga la Covid-19,” amesema Profesa Aboud.
0 Comments