Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Wilaya ya Kinondoni ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha zoezi la kupandisha vyeo/madaraja walimu 1,333 wa shule za msingi na sekondari wa Manispaa ya Kinondoni ambao wana sifa za kupanda vyeo kwa mujibu wa miongozo na taratibu za Serikali.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Katibu Msaidizi wa TSC wa Wilaya hiyo, Theobald Kilindo wakati akitoa taarifa kwa Mkurugenzi wa Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC Makao Makuu, juu ya hatua iliyofikiwa katika zoezi la kuwapandisha vyeo walimu wa Manispaa hiyo, ambapo ameeleza kuwa ofisi yake imepitia hatua mbalimbali katika kufanya zoezi hilo, na kila hatua ilifanyika kwa uangalifu.
“Tuliletewa barua na Mkurugenzi iliyotutaka tuanze zoezi la kupandisha vyeo walimu. Tuliitisha majalada yote ya walimu na kuanza kuyachambua ili tuweze kubaini walimu wenye sifa za kupanda vyeo. Tulianza zoezi la uchambuzi Mei 3 na kulihitimisha Mei 11,” alisema Kilindo.
Kilindo ameeleza kuwa uchambuzi ulipokamilika walipitia Ikama ya walimu ya miaka mitatu (2018/2019, 2019/2020 na 2020/2021) na kuona kuwa Manispaa hiyo ina jumla ya nafasi 2874 za kupandisha vyeo walimu katika madaraja mbalimbali.
“Baada ya taratibu zote kukamilika, Kamati ya TSC Wilaya ambayo ndiyo yenye wajibu kisheria wa kupandisha vyeo walimu, ilifanya kikao chake Mei 12, 2021 na kuwapandisha vyeo walimu 1,333 ambao ndio waliokuwa na sifa,” alifafanua Kilindo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Christina Hape alisema kuwa Serikali ilifanya jambo la busara kwa kuamua kuchukua Ikama za miaka mitatu kwa kuwa hatua hiyo inaondoa kabisa malalamiko ya madaraja kwa walimu, huku akitoa wito kwa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kujitahidi kuwabadilishia mishara walimu mapema iwezekanavyo.
“Unajua ukimwambia mwalimu umepanda cheo anataka aone mshahara umebadilika, kumpatia karatasi (barua) ya kupanda cheo peke yake bila yeye kuona maslahi yake yameboreshwa haitakuwa na faida sana kwake. Hivyo, napenda niwaombe wenzetu wa UTUMISHI kuhakikisha wanafanya kila linalowezekana ili mishahara ya walimu iendane na vyeo vyao kwa wakati,” alisema Mkurugenzi huyo.
Manispaa ya Kinondoni ina Jumla ya walimu 2,922 wa shule za msingi na sekondari wanaofundisha shule za Serikali, ambapo katika idadi hiyo, walimu 1939 ni wa shule za msingi na walimu 983 ni wa sekondari.
0 Comments