F Dkt Ndugulile ataka makampuni ya simu kulinda siri za wateja wao | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Dkt Ndugulile ataka makampuni ya simu kulinda siri za wateja wao


Na Ezedkiel Mtonyole – Dodoma.

Makampuni ya simu yanayotoa huduma za mawasiliano hapa nchini yametakiwa kuboresha   huduma wanazotoa kwa wateja pamoja na  kushushughulikia changamoto ya matumizi sahihi ya

vifurushi  pamoja na kukomesha tabia ya baadhi ya wafanyakazi wa makampuni hayo kuvujisha  siri za wateja.

Wito huo umetolewa Jijini Dodoma na Waziri wa mawasiliano na teknolojia ya habari, Dkt.Faustine Ndugulile wakati akizungumza na wawakilishi wa makampuni hayo kikao kilichokuwa na lengo la kujadiliana namna bora ya kupeleka mawasiliano katika maeneo ambayo hayana huduma ya mawasiliano.

Waziri Dkt Ndugulile amesema anataka kuona makampuni hayo yanafanya maboresho kwa kuhakikisha wanashughulikia changamoto hiyo ikiwa ni pamoja na kulinda siri za wateja pamoja na kuweka mifumo imara ya kusajili namba mpya za simu.

“Kama serikali tulitaka kuwaondoa mawakala wa kusajili laini lakini baada ya kufikilia tukaona ni kundi kubwa mno la wananchi wanaotoa huduma ya kusajili line, hivyo tukasitisha zoezi hilo, lakini mawakala hawa wawekewe utaratibu mzuri kwani baadhi yao si waaminifu mkawasimamie” amesema Dkt Ndugulile.

Waziri Ndugulile pia amesema Serikali itaendelea kutoa ruzuku

kwa makampuni hayo ili yaweze kupeleka huduma ya mawasiliano katika maeneo ya mipakani mwa nchi yaweze kufikiwa na huduma ya mawasiliano.

Aidha Waziri Ndugulile amepiga marufuku kwa kampuni yoyote kwa sasa kujenga mkongo bila ya kuomba kibali kutoka wizarani kwani serikali ndio inayojenga mkongo wa taifa.

kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa mfuko wa mawasilino kwa wote,(UCSAF) Justina Mashiba amesema  lengo la kikao hicho ni  kuangalia namna bora ya kupeleka mawasiliano maeneo ambayo hayana mawasiliano kwani lengo la mfuko huo ni kupeleka mawasiliano kwa wote.

“watoa huduma tunahitaji kupeleka mawasiliano nchi nzima na tutatoa zabuni kuhakikisha mawasiliano yanafika mpaka katika maeneo ya vijijini hasa maeneo ya mipakani” amesema.

Naye Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasilino na Teknolojia ya

Habari Kundo Andrew amesema kwa sasa mawasiliano ni chakula hivyo kila mtanzania anahitaji kupata mawasiliano hata ambaye yupo kijijini.

amesema ndio maana wanatoa ruzuku kwa makampuni hayo lengo likiwa kila mtanzania aweze kupata mawasiliano huku akisisitiza serikali ipo tayari kushirikiana na watoa huduma hao ili wananchi waweze kunufaika.

Nao baadhi ya wawakilishi wa Makampuni ya simu Andrew Lupembe kutoka Vodacom na Emmanuel Mallya wamesema wapo tayari kushirikiana na serikali na taasisi zake katika kuhakikisha wanatoa huduma bora za mawasiliano na wanaendelea na jitihada za kuhakikisha wanakomesha vitendo vya wizi mitandaoni.


Post a Comment

0 Comments