Na Omary Mngindo, Mlandizi.
LIGI Kuu ya soka Tanzania Bara imeendelea jioni hii kwenye uwanja wa JKT Ruvu Mlandizi mkoani Pwani, kati ya Ruvu Shooting na Polisi Tanzania ambapo zimetoka sare ya bao 1-1.
Katika mchezo huo iliokuwa mkali kwa muda wote wa dakika tisini, Shooting walianza kupata bao kunako dakika ya 34 kwa bao safi likifungwa na David Ulomi, akitumia vema makosa ya mabeki wa timu ya Polisi, mpira ukimpita kipa Geoffrey Mkumbo.
Baada ya bao timu zote zilishambuliana kwa zamu, ambapo kunako dakika ya 57 Polisi walisawazisha kupitia Tariq Seif akiunganisha mpira wa krosi kutoka wingi ya kushoto iliyopigwa na Kassimu Haaruna
Timu hizo zinazonolewa na Charles Boniface "Mkwasa" upande wa Shooting na Malale Hamsini wa Polisi Tanzania, zilishambuliana kwa zamu huku wakifanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji ambayo hata hivyo hayakuweza kubadili matokeo.
Shooting ilifanya iliwampumzisha Banka nafasi yake ikachukuliwa na Emmanuel Martine, Fulluzulu Maganga akampisha Samson Kwakwala, huku Polisi wakiwapumzisha Deusdedit Okoyo na Tariq Seif nafasi zao zikichukuliwa na Marcel Kapama na Shaaban Stambuli.
Kwa upande wao makocha Mkwasa na Hamsini wamepokea matokeo hayo kila mmoja akisema kwamba anakwenda kuyafanyiakazi mapungufu yaliyojitokeza ili wapate matokeo mechi zijazo.
0 Comments