F SMZ imetoa ruhusa ya maombi ya kukodishwa majengo ya mji mkongwe | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

SMZ imetoa ruhusa ya maombi ya kukodishwa majengo ya mji mkongwe


Na Thabit Madai,Zanzibar.

SERIKALI  ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa ruhusa ya kutangaza maombi ya  kukodishwa kwa majengo ya Mamlaka   ya uhifadhi na uendelezaji wa Mji Mkongwe kwa nyumba za Serikali na binafsi ili kuimarisha soko la Utalii nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Kikwajuni Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Lela Mohamed Mussa wakati akiwasilisha vipaumbele vya Wizara kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kuhusu Mamlaka ya Uhifadhi na Uendeshaji wa Mji Mkongwe.

Alisema kuwa Serikali imefanya maamuzi ya kutangaza rasmi maombi kwa ajili ya kuwekeza na kukodisha ndani ya Mji huo katika majengo yote ya Serikali na miundo mbinu mbalimbali iliyomo ndani ya eneo la uhifadhi.

Alifahamisha kwamba,  maombi hayo yatakuwa yanatangazwa awamu kwa awamu mpaka pale lengo la kuona mji huo umeimarika majengo na miundombinu yake ili kuwa kivutio bora nchini ambapo kwa awamu ya kwanza maombi yataanza kupokelewa kuanzia leo hadi Julai (9) tisa mwaka huu.

“Fomu za maombi zinapatikana katika website ya Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale www.utaliism.go.tz.”, alieleza Waziri Lela.

Alisema Mji Mkongwe ni urithi wa Dunia  hivyo jukumu la Serikali  kuhakikisha urithi  huo unabaki na kuendelea kufaidisha wananchi wa visiwa vya Zanzibar na vizazi vijavyo.

Waziri Lela alieleza kwamba kwa sasa  mamlaka ya Mji Mkongwe   imekamilisha rasimu ya mpango wa  uhifadhi ya mji huo ambayo kwa kiasi kikubwa inaakisi umaarufu unaotokana na historia ya majengo ya kihistoria na utamaduni wa WazanzibarI ambao ni kivutio cha utalii na biashara kwa Zanzibar.

Aliongeza kuwa, katika bajeti ya Serikali  imejipanga kutekeleza kuimarisha taasisi zake ikiwemo  sekta ya utalii kwa kuwapa kipaumbele ikiwemo kufanya utafiti wa kutambua uwezo wa visiwa vya Zanzibar wa kuhimili idadi ya wageni wanaoingia nchini.

Vile vile alifahamisha kuwa  katika kuendeleza utalii kwa kutoa elimu juu ya dhana za utalii kwa rika zote hasa Pemba kupitia masheha , maskulini, maonesho mbalimbali na makongamano ya utalii kitaifa na kimataifa ili kuvutia wageni.

Hata hivyo Waziri Lela aliwapongeza  wananchi kwa kuunga mkono Serikali kwa lengo la kuhakikisha inaimarisha hali ya wananchi wake katika kuwaletea fursa mbalimbali za maendeleo.

 

Post a Comment

0 Comments