Waziri Ummy atoa maelekezo mazito kwa watendaji Serikalini


Serikali imewaagiza Watendaji wa Halmashauri nchini kuhakikisha wana kusanya mapato kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni na kwamba fedha zote ziwekwe benki kupitia mifumo ya kielektroniki ndani ya masaa 24.


Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI) Mheshimiwa Ummy Mwalimu katika Halmashauri ya Wilaya Igunga wakati akiongea na Watendaji wa Halmashauri, baadhi ya Viongozi wa Mkoa wa Tabora, Kamati tendaji ya Halmashauri ya Igunga, Waheshimiwa Madiwani na baadhi ya watendaji kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI.


Waziri Ummy Mwalimu amesema katika Halmashauri ya Igunga fedha inaonekana inapelekwa benki lakini mapato yanayoonekana ni kidogo kwa kuwa mifumo ya kielektroniki haitumiki ipasavyo kwa kuwa fedha zinaliwa kabla hazijaingia benki kutokana na kisingizio cha kuharibika kwa mashine za kukusanyia mapato au kutokuwepo kwa mapato kwenye baadhi ya maeneo.


“tuzingatie maelekezo ya Serikali, ya kukusanya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa kutumia mifumo ya kielektroniki, kwa kuhakikisha mapato ya ndani yaliyokusanywa yanawasilishwa benki ndani ya  masaa 24 kabla hayajatumika, waheshimiwa Madiwani, Kamati ya fedha hii ni kazi yetu tunatakiwa kuhakikisha tunasimamia ipasavyo ukusanyaji wa mapato” 


Aidha, Waziri Ummy Mwalimu amewataka Viongozi na Watendaji wote wa Halmashauri kudumisha ushirikiano lakini watimize wajibu wao kusimamia mapato na matumizi ya fedha za Halmashauri  kwani itasaidia kuweka sawa mahesabu ya fedha na kupunguza hoja za ukaguzi

Post a Comment

0 Comments