F Ijue historia ya soko la Kariakoo | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Ijue historia ya soko la Kariakoo

 


Soko Kuu la Kariakoo lipo katika kiwanja namba 32 mtaani Kariakoo, katikati ya makutano ya mtaa wa Mkunguni na mtaa wa Nyamwezi na limezungukwa na mitaa ya Nyamwezi, Mkunguni, Sikukuu na Tandamti.


Historia ya soko la Kariakoo inarudi nyuma hadi enzi za Wakoloni wa Kijerumani wakati wanaitawala Tanganyika.


Awali Wajerumani walikusudia kujenga ukumbi wa kuadhimisha sherehe za kutawazwa kwa Mfalme Kaiser Wilheim wa pili wa Ujerumani kwa wakati huo.


Kaisari Wilhelm II alikuwa mfalme wa mwisho wa Prussia na kaisari wa mwisho wa Ujerumani kuanzia mwaka 1888 hadi 1918.


Hata hivyo baada ya jengo kukamilika halikutumiwa kama ilivyokusudiwa kuwa na badala yake lilitumika kama kambi ya kikosi cha wapagazi waliobeba mizigo ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia waliojulikana kama 'Carrier Corps'.


Jina hilo ndilo lililokuja kuzaa neno Kariakoo, kwani Waswahili hawakuweza kutamka Carrier Corps, walilitohoa.


Baada ya Vita Kuu ya Dunia kwisha mwaka 1919 na Wajerumani kuondoka, Tanganyika ikaanza kutawaliwa na Waingereza, jengo hilo lilianza kutumika kama soko na kuhudumia wakazi wa Dar es Salaam, ambapo wafanyabiashara walikuwa wakiuza bidhaa zao sakafuni kwa sababu hapakuwa na meza hadi mwaka 1960, meza za saruji zilipojengwa.


Kutokana na ongezeko la watu jijini Dare s Salaam, kulikuwa na msongamano mkubwa watu sokoni hapo na hivyo soko hilo kushindwa kuhudumia wafanyabiashara.


Ndipo mwaka 1970, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam iliagiza kujenga Soko jipya la kisasa ambalo lingechukua nafasi ya soko la zamani. Uamuzi huo ulianza kutekelezwa Machi 1971.


Ramani ya jengo la soko ilitayarishwa na mchoraji wa ramani za majengo Mtanzania Beda Amuli. Mchoraji huyo alikuwa Mwafrika wa kwanza kwa Afrika Mashariki na Kati kuwa na ofisi yake binafsi ya utaalamu wa ujenzi tangu mwaka 1969.


Baadhi ya taarifa zinasema, mkandarasi huyo alitakiwa kwenda kujifunza nchi za Accra nchini Ghana na Lusaka nchini Zambia, kuangalia masoko yaliyojengwa katika miji hiyo miwili, ndipo atengeneze ramani yake, lakini mwenyewe aliwahi kusema kuwa alipata wazo la kutengeneza ramani ya jengo hilo kutokana na utaalamu alioupata nchini Israel alikosomea.


Amuli alifariki Julai 10, 2016, tarehe hiyo hiyo ndiyo soko la Kariakoo limeunga.


Ujenzi wa soko ulikamilika mwaka 1975 kwa gharama ya Sh22 milioni na kufunguliwa rasmi Desemba mwaka huo huo, na Rais Julius Nyerere akiwa mgeni rasmi.


Soko hilo Lina majengo mawili amvato yameunganishwa katika ghorofa ya chini ya ardhi. Soko kubwa limegawanyika katika sehemu tatu ambayo ni ghorofa ya kwanza, sehemu ya kati na ya chini maarufu kama shimoni.


Imgawa eneo la Kariakoo limezungukwa na maduka yanayouza bidhaa mbalimbali, bado Soko la Kariakoo ndiyo soko kuu la mauzo na bidhaa za Kilimo nchini. Linauza mazao kwa bei ya jumla na ya rejareja pamoja na vifaa vya Kilimo.

Post a Comment

0 Comments