F Mkandarasi ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme mradi wa JNHPP aanza kazi | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Mkandarasi ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme mradi wa JNHPP aanza kazi

Imeelezwa kuwa, Mkandarasi atakayejenga njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kV 400 kutoka eneo la mradi wa umeme wa Julius Nyerere ( JNHPP), Rufiji mkoani Pwani hadi Chalinze ameanza kazi.


Hayo yametanabaishwa wakati wa ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Adolf Ndunguru  pamoja na  Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali mkoani Dar es Salaam na Pwani iliyolenga kukagua maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya kupoza umeme utakaotoka katika Bwawa la Umeme la Julius Nyerere.

Viongozi hao waliambatana na Makamishna na Wakurugenzi wa Idara mbalimbali kutoka Wizara hizo mbili pamoja na watendaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO- Uwekezaji, Khalid  James alisema kuwa,  ujenzi wa njia hiyo ya kusafirisha umeme itakuwa na urefu wa kilometa 160 na kwamba wananchi takriban 300 waliopisha maeneo yatakapojengwa miundombinu hiyo ya usafirishaji umeme wameshalipwa fedha zao na hivyo wamebaki takriban wananchi 100 tu kulipwa fidia.

Alitaja kampuni inayotekeleza mradi huo kuwa ni  Larsen & Toubro  kutoka India.

Aliongeza kuwa,  katika eneo la Chalinze kutajengwa kituo kipya cha kupoza umeme unaotoka katika mradi huo wa Julius Nyerere ambacho  kitakuwa na transoma Sita ambapo transfoma Nne zitapoza umeme kutoka kV 400 kwenda kV 220 na  transfoma nyingine Mbili zitapoza umeme  hadi kV 132 .

Alieleza kuwa mpaka sasa wameyatambua maeneo ya kulipa fidia wananchi waliopisha maeneo yao kupisha ujenzi wa kituo hicho na kwa sasa wanakamilisha taratibu za  mwisho kabla ya kuanza kulipa fidia.

Wakiwa  mkoani Dar es Salaam Viongozi hao walikagua eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo kipya cha kupoza umeme katika eneo la Kinyerezi ambapo Mhandisi  mradi kutoka TANESCO, Deogratius Nyamtumbega alisema kuwa, kituo hicho kitakuwa na msongo wa kilovoti 400.

Alieleza kuwa, katika kituo cha Kinyerezi  kutakuwa na transfoma nne za 250 MVA ambazo zitapoza umeme kutoka kV 400 kwenda kV 220 ambapo kituo hicho kitasambaza umeme katika maeneo mbalimbali nchini kulingana na mahitaji.

Baada ya ukaguzi wa maeneo hayo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Adolf Ndunguru alishukuru Wizara ya Nishati na TANESCO kwa kuwaonyesha viongozi hao kutoka Wizara ya Fedha kile kinachotekelezwa na Serikali kwa sasa ili waone maendeleo yake.

Aidha,  ametoa wito kwa Taasisi hizo kufanya kazi kwa pamoja ili mradi huo wa kimkakati usikwame.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali alieleza kuwa,  Wizara  ya Nishati na TANESCO zimefarijika kwa viongozi hao wa Wizara ya Fedha kutembelea  mradi wa umeme wa Julius Nyerere kwani hiyo ni mdau muhimu katika utekelezaji wa mradi huo.

Alitoa wito kwa viongozi wa Wizara hiyo kutembelea miradi mingine ya kimkakati inayosimamiwa na Wizara ya Nishati. 

Viongozi hao kutoka Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Wizara ya Nishati, walitembelea pia mradi wa uzalishaji umeme kwa kutumia gesi asilia wa Kinyerezi II ambao unazalisha umeme wa kiasi cha megawati 240.

 

Post a Comment

0 Comments